25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi 600 kunufaika na elimu ya utambuzi kutoka FTT

Na Clara Matimo, Mwanza

Jumla ya wasichana 600 kutoka shule za msingi na sekondari Wilayani Ilemela mkoani Mwanza wanatarajia kunufaika kwa kupata elimu tambuzi kupitia mradi wa Msichana Thabiti utakaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na maendeleo kwa vijana, Fadhili Teens Tanzania (FTT).

Msimamizi wa Mradi wa Msichana Thabiti, Sarah Emmanuel(aliyesimama) akizungumza na viongozi wa Kata ya Nyasaka Wilayani Ilemela wakati akitambulisha mradi huo.

Mradi huo pia utawanufaisha wasichana ambao wako nje ya shule waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito au maradhi hivyo kushindwa kufikia ndoto zao na kuzitimiza.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na Afisa Programu Msaidizi wa FTT, Anitha Modesti wakati akitambulisha mradi huo kwa viongozi wa Kata ya Nyasaka ambako utatekelezwa na kufafanua kwamba utawafikia wasichana 400 wa shule ya Sekondari Nyasaka na 200 wa Shule ya Msingi Muungano.

Kwa mujibu wa Anitha lengo kuu la mradi huo ni kukuza ustawi wa wasichana walioko ndani na nje ya shule kwa kuwapa elimu tambuzi ili wajitambue waweze kupata taarifa sahihi.

“Mradi  wa Msichana Thabiti unalenga kuwajengea uwezo wasichana walioko shuleni na walio nje ya shule ambao walikatisha  masomo  kutokana na sababu mbalimbali ili wajitambue na kufikia malengo yao.

“FTT tunaamini kwamba kama msichana alipata ujauzito akakatisha masomi inamaana tayari ni mzazi ingawa na yeye bado ni mtoto hivyo hao ambao wako nje ya shule na wamekwishakuwa wazazi tutawakutanisha na fursa mbalimbali za kijamii zinazoleta maendeleo kiuchumi ili wafikie malengo yao pia waweze kujihudumia wao na watoto wao,” alisema Anitha na kuongeza.

“Walioko shuleni tutaongea nao mada tofauti tofauti kulingana na umri wao tunachohitaji ni kuibua vipaji vyao waweze kufikia ndoto zao, tumeamua kuleta mradi huu Kata ya Nyasaka kwa sababu ofisi zetu ziko hapa tunatekeleza mradi huu Wilaya za Magu, Misungwi na Sengerema Mkoani Mwanza tumebaini changamoto zinazowakabili wasichana zinasababishwa na ukosefu wa elimu tambuzi hawajui mambo yapi hawapaswi kufanya wakiwa wanasoma,” alifafanua Anitha.

Anitha alieleza kwamba ili kukabiliana ma mmomonyoko wa maadili katika jamii inapasa makundi yote kushirikiana kuwalea watoto kuanzia wazazi, viongozi wa kada zote ikiwemo wa dini, serikali, siasa, taasisi  za serikali na zisizo za serikali.

Msimamizi wa mradi huo Sarah Emmanuel alisema kupitia mradi huo watawafikia wasichana 10 walioko nje ya shule ambapo  watawaunganisha na mashirika mengine wanayofanya nayo kazi ili yawasaidie waweze kufikia malengo yao kwa kuwa msichana au mama mwenye mtoto katika umri mdogo anakuwa na mahitaji mengi zaidi.

“Hivyo kupitia mradi wa Msichana Thabiti tutawapa elimu na kuwawezesha ili waweze kujishughulisha na biashara zitakazowaingizia kipato waweze kujisaidia wenyewe, watoto wao na familia zao pia tutawaunganisha na fursa mbalimbali ambazo zipo ndani ya jamii lakini hawafahamu kama zinaweza zikawasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazowakabili,” alifafanua Sarah.

Kwa upande wao  baadhi ya walimu wa shule  ambazo zitanufaika na mradi huo akiwemo mwalimu wa Malezi katika shule ya Sekondari Nyasaka  Frida Biseko na Mwalimu wa  Afya na Malezi Shule ya Msingi Muungano Monica msagala walisema mradi huo utwawasaidia watoto wa kike  kwa sababu katika jamii ndio wanaopata changamoto nyingi sana za kimaisha.

“Binafsi nalishukuru sana Shirika la  Fadhili Teens Tanzania kwa kuleta mradi wa Msichana Thabiti katika Kata yetu  hasa katika shule ya Sekondari Nyasaka, nikiwa mwalimu wa malezi shuleni hapo naamini mradi huu utawasaidia sana wanafunzi wa kike maana mara  nyingi tunasikia ama tunaona wasichama wakifanyiwa ukatili mbalimbali ikiwemo kubebeshwa mimba ambapo inawalazimu kakatisha masomo,”alisema Mwalimu Frida.

“Imani yangu ni kwamba watoto wa kike wataweza kutimiza ndoto zao kwa sababu elimu tambuzi itawasaidia kujua jambo gani wanapaswa kufanya na lipi wasifanye na kwa wakati gani,”alisema Mwalimu wa Afya na Malezi Shule ya Msingi Muungano, Monica msagala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles