CHRISTINA GAULUHANGA NA BERTHA MWAMBALASWA (MSPS), DAR ES SALAAM
HATIMAYE Serikali imewakumbuka wanafunzi 269 kati ya 290 walioachwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kuwapangia vyuo waweze kuendelea na masomo yao.
Hata hivyo, wanafunzi 21wataendelea kusota mitaani kwa vile walipata daraja IV katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha nne.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, alisema wizara ilitafakari kwa kina baada ya kupokea maombi mengi kutoka kwa wanafunzi hao ambao walionyesha nia ya dhati ya kusomea ualimu.
Alisema idadi hiyo ni miongoni mwa wanafunzi walioachwa awali ambao walikuwa ni 1,471 waliokuwa wanachukua stashahada ya sekondari na msingi huku baadhi yao wakibainika kukosa vigezo vya kusomea kozi hiyo.
Dk. Akwilapo alisema katika programu ya kwanza, wanafunzi 6, 595 walidahiliwa kusoma programu maalumu iliyowaandaa kwenda kufundisha katika shule mbalimbali za sekondari .
Alisema Serikali ilibaini 6, 305 ndiyo wenye sifa stahiki za kufundisha ngazi hiyo huku wenye ufaulu wa daraja la kwanza na la pili walirejeshwa kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Baada ya Serikali kufanya uchambuzi, wanafunzi waliobaki awali ambao wamebainika wana sifa wamepangiwa kuendelea na masomo katika vyuo vingine vya serikali vya Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kwa mwaka wa kwanza na wa mwaka wa pili watamalizia masomo katika vyuo vya Korogwe na Kasulu,” alisema Dk.Akwilapo.
Alisema wanafunzi 1,181 waliochwa awali ambao walikuwa wanasomea ualimu wa shule ya msingi, waliagizwa waombe mafunzo yanayolingana na sifa zao kupitia Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE), ambao tayari wamepangiwa vyuo kulingana na sifa zao.
Dk. Akwilapo alisema wanafunzi wanaoendelea na masomo yao UDOM Serikali itaendelea kuwapa mikopo ya kufadhili masomo yao na ambao wamepangiwa vyuo vya ualimu vya serikali watalipiwa mkopo wa ada tu.
Mitihani darasa la nne
Dk. Akwilapo alisema wizara inaendelea na maandalizi ili wanafunzi wa vyuo waanze masomo Oktoba 15, mwaka huu na kusisitiza kuwa utaratibu wa mitihani ya darasa la nne na kidato cha pili utaendelea kama kawaida.
“Wanafunzi ambao hawatafikia viwango vya ufaulu wa mitihani hii ya kujipima watatakiwa kukariri darasa au kidato,” alisema.
Uamuzi wa awali
Julai 19, mwaka huu, Serikali ilitangaza kuwaondoa rasmi wanafunzi 1,500 na kuwahamishia katika vyuo vingine vya ualimu wanafunzi 5,913 kati ya 7,805 waliokuwa wanasomea stashahada maalumu ya ualimu wa shule za msingi na sekondari kwa masomo ya sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).