Vilio, simanzi vyatawala vifo vya polisi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akitoa heshima za mwisho mbele ya majeneza yenye miili ya askari waliouawa na majambazi Dar es Salaam jana katika eneo la Mbande, Mbagala.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akitoa heshima za mwisho mbele ya majeneza yenye miili ya askari waliouawa na majambazi Dar es Salaam jana katika eneo la Mbande, Mbagala.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akitoa heshima za mwisho mbele ya majeneza yenye miili ya askari waliouawa na majambazi Dar es Salaam jana katika eneo la Mbande, Mbagala.

JOHANES RESPICHIUS, DAR ES SALAAM

VILIO, simanzi na huzuni jana vilitawala wakati wa kuaga miili ya askari polisi wanne waliouawa  na watu wanaodaiwa kuwa majambazi baada ya kuvamia Tawi la Benki ya CRDB lililopo Mbande, wilayani Temeke, Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kuaga miili ya marehemu hao katika Viwanja vya Polisi Barracks barabara ya Kilwa kwa heshima zote za kijeshi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema ni vema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ikaweka utaratibu wa kuzijengea nyumba  familia za marehemu wanaopoteza uhai wakati wakilitetea taifa.

“Nitoe rai kwa nchi yetu kuweka  utaratibu kwa askari yoyote anayepoteza  uhai katika mapambano angalau familia yake ijengewe nyumba kama sehemu ya kumbukumbu ili hawa ndugu wasibaki wapweke,” alisema Makonda.

Akito salamu za Rais Dk. John Magufuli, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu alisema ameguswa na msiba huo na kutoa pole kwa familia za ndugu na jeshi kwa kuondokewa na askari hao.

IGP Mangu alisema kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli ametoa rambirambi ya Sh milioni 10, ambazo zitagawiwa kwa familia zote zilizopoteza ndugu zao.

IGP Mangu alisema kwa upande wake jeshi hilo, huwa na utaratibu wa kutoa rambirambi ya Sh milioni 15 kwa kila askari anayepoteza uhai.

“Napenda kuchukua nafasi hii, kuwaomba ndugu wa marehemu baada ya kumaliza shughuli za msiba wafike makao makuu ya jeshi la polisi ili kuanza taratibu za kupewa fedha hizo na kushughulikia mirathi.

“Pia nawatia moyo askari polisi tuendelee kupambana na wale wanaotafuta nguvu za kupambana na sisi, tujipange vizuri kupambana nao zaidi,’alisema IGP Mangu.

Kwaupande wake Benki ya CRDB ilitoa rambirambi ya Sh milioni 2 kwa kila familia ya marehemu.

Meneja Mkuu wa benki hiyo, Sebastian Masaki alisema wameguswa na tukio hilo, kwa sababu kuna familia za marehemu zimeachwa bila kitu.

“Mbali na fedha hizi, tumeamua kutoa Sh milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi cha kisasa pale Mbande,”alisema.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, licha ya kutoa pole kwa familia zilizofiwa na wapendwa wao na kumweleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira,  kupitia upya sheria na kuangalia namna bora ya kuwawekea bima ya maisha kwa askari wote.

“Naelekeza kuangalia upya sheria na namna bora ambayo tutaweka bima ya maisha kwa askari wote na kabla ya sheria hii kuangaliwa wizara itakuwa karibu na familia za marehemu na tutaomba mawasiliano yao,” alisema Waziri Nchemba.

Pia alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea kuwasaka, kuwakamata na kuwatia mbaroni majambazi hao ikiwa ni pamoja na watu walioandika kwa kejeli kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mauaji hayo.

Alisema ni lazima jeshi lichunguze uhusiano uliopo kati ya watu wanaoshabikia tukio hilo kwenye mitandao na majambazi walioua askari hao iwe ni kwa mlengo wa kisiasa kwa sababu hawakuwa katika makao makuu ya chama chochote.

Askari hao waliuawa kwa kupigwa risasi juzi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi wakati askari hao, wakienda kubadilishana zamu na wenzao.

Katika tukio hilo, askari waliouawa ni  E.5761 Koplo Yahaya, F. 4660, Koplo  Hatibu, G. 9524 PC Tito na  G.9992 PC Gastone, huku raia wawili Ally Chiponda na Azizi Yahaya wakijeruhiwa.

Licha ya kuuawa kwa askari hao, majambazi hao walipora silaha bunduki mbili aina ya Sub Machine Gun (SMG) na risasi 60.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here