NA RAYMOND MINJA, IRINGA
ZAIDI ya wanafunzi 100 wa Shule ya Msingi Image wilayani Kilolo, wanalazimika kukaa darasa moja kutokana na upungufu wa madarasa uliochangiwa na uchakavu wa majengo ya shule hiyo.
Shule hiyo yenye wanafunzi 761 inahitaji vyumba 18 vya madarasa lakini hadi sasa ina vyumba tisa na vyumba vitatu tu ndivyo vinatumika.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Osideus Lukas, alisema hayo jana baada ya kupokea msaada wa mabati 50 kwa ajili ya kuezeka madarasa mawili.
Mabati hayo yalitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa huo, Jesca Msambatavangu.
Lukas alisema hali ya shule hiyo kwa sasa si ya kuridhisha kutokana na uchakavu wa majengo.
Alisema hivi karibuni Idara ya Ukaguzi ya Kanda ilivifunga vyoo vya wanafunzi wa kiume vya shule hiyo kwa kuwa vimejaa na wanafunzi hao kulazimika kutumia vyoo vya wanafunzi wa kike.
“Shule yetu ina mazingira magum,u kwa kweli tunahitaji watu wengine kama alivyoguswa huyu mama.
“Mbali na madarasa pia tuna uhaba wa vyoo kwa sababu hivi karibuni wakaguzi walikuja na kutuamuru kufunga vyoo vya wavulana kwa kuwa vilikuwa vimejaa hivyo kwa sasa wavulana wanatumia choo kimoja na wasichana,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo, Petro Mkenja alisema mabati hayo yatasaidia kuezeka jengo la vyumba viwili vya madarasa lililokuwa wazi.
Aliwataka watu wengine kuiga mfano wake katika kusaidia jamii.