Na Mwandishi Wetu, Monduli
VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wamemwomba Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), kuchukua fomu ya kuwania urais muda utakapofika kwani wanaamini ni kiongozi anayefaa kuwania nafasi hiyo kupitia chama hicho.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Vicent Nyamasagi, viongozi hao walitoa kauli hiyo jana Monduli baada ya kufika nyumbani kwa Lowassa kuwasilisha ombi hilo.
Lakini pamoja na viongozi hao kuwasilisha ombi hilo, Lowassa hakutoa jibu la kukubali wala kukataa na badala yake alirejea kauli yake kwa kusema kuwa suala hilo ni kubwa, linahitaji maombi na baraka za Mwenyezi Mungu.
“Historia yako inaonyesha ni mtu mwenye uwezo wa kufanya maamuzi magumu, mapana na sahihi kwa masilahi ya nchi yetu.
“Kwa hakika una sifa zote za kuwa rais wa nchi yetu, tunakuomba muda ukifika chukua fomu, wananchi wana imani kubwa na wewe,” alisema Nyamasagi.
Aliongeza kuwa Watanzania wameshuhudia uwezo mkubwa wa Lowassa katika nafasi zote alizowahi kushika na ndiyo maana jina lake sasa ni tumaini pekee la wananchi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) wa Wilaya ya Serengeti, Patric Marwa, alisema hakuna kiongozi yeyote ndani ya CCM anayefanana na Lowassa kuweza kushika nafasi hiyo.
“Hakuna kiongozi mbadala wa Lowassa kwa sasa, anajua historia ya chama chetu na nchi, katika maisha yake yote ya utumishi amekitumikia chama kwa uadilifu mkubwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, John Ng’oina, alisema wana imani na Lowassa na kuwa atasikia kilio cha Watanzania kumtaka achukue fomu kuwania urais.
Hatua hiyo ya viongozi hao imekuja kutokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Februari Mosi mwaka huu ya kutaka wana CCM wenye uwezo washawishiwe wachukue fomu ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi ndani ya CCM.