28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Upinzani wambeba Prof. Mwandosya urais 2015

Mwandosya-MarkNA GORDON KALULUNGA, MBEYA
VIONGOZI wa Chama cha NCCR-Mageuzi na TADEA mkoani hapa, wamemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, kugombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba ni mtu mwadilifu.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mbeya, viongozi hao walisema wamechoshwa na tetesi na minong’ono iliyopo mitaani kuwa atawania nafasi hiyo huku yeye akiwa amekaa kimya bila kukata kiu ya wafuasi wake ndani na nje ya CCM.
Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Mbeya, Chifu Daimon Mwakatumbula, alisema wanamtaka Profesa Mwandosya kutangaza msimamo wake akiwa mkoani Mbeya ambako ni Mbunge wa Rungwe Mashariki.
“Tunamtaka Profesa Mwandosya aje Mbeya na atangaze akiwa huku kuhusu msimamo wake wa kuwania nafasi ya urais mwaka huu au la, na sisi akitangaza kuwania nafasi hiyo tutamuunga mkono maana ni mwadilifu,” alisema Chifu Mwakatumbula.
Akizidi kumpigia debe, Mwakatumbula alisema katika wizara ambazo amewahi kuongoza Profesa Mwandosya hajawahi kuwa na kashfa na kwamba hana tabia ya kusaidia mtu mmoja mmoja bali anakuwa na masilahi mapana ya taifa.
“Sisi kama viongozi wa vyama vya upinzani, tunamtafuta rais wa nchi na wala siyo rais wa chama fulani, kwa sababu tunaamini katika kaulimbiu ya ‘Tanzania kwanza, vyama baadaye’,” alisema Mwakatumbula.
Kiongozi huyo ambaye chama chake kimo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wanatarajia kusimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu ujao, alisema mwaka 2010, hata Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba aliwahi kusema Mwandosya ndiye anafaa kuwania urais.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TADEA Mkoa wa Mbeya, Boniface Mwakibinga, alisema Profesa Mwandosya kabla hajawa Mbunge wa Rungwe Mashariki, alidhihirisha kuwa uongozi huanzia nyumbani baada ya kujenga shule na kupeleka maji katika jimbo lake.
“Profesa Mwandosya ni msikivu na ana heshima kubwa kwa wenzetu wa nje ya nchi kutokana na uadilifu wake, hivyo akipata nafasi ya urais hakika Tanzania tutakuwa tumepata kiongozi bora na sisi wapinzani tutampigia kura bila kujali itikadi zetu,” alisema Mwakibinga.
Kwa upande wake aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, kupitia NCCR-Mageuzi, Policia Mwaiseje, alisema baadhi ya waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wana harufu mbaya za ufisadi.
“Maandiko matakatifu yanasema tafuteni kwanza ufalme wa mbinguni na mengine yote mtazidishiwa, lakini kwenye siasa ni kwamba tafuteni kwanza ufalme wa siasa na mengine yote mtayapata, hivyo mapinduzi ya kiutamaduni yanahitajika katika taifa ili tusonge mbele,” alisema Mwaiseje.
Kuhusu yeye kuwania ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini, alisema hadi sasa hajafanya uamuzi ingawa atamuunga mkono mgombea yeyote atakayesimamishwa na Ukawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles