26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Sekta ya utalii yaingiza dola bilioni 2 kwa mwaka

Gavana nduluNA ADAM MKWEPU DAR ES SALAAM
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, amesema sekta ya utalii nchini inaongoza kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni na kufikia dola za Marekani bilioni 2 kwa mwaka kutokana na hali ya mabadiliko ya mfumo wa mapato hayo.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa mwaka ulioandaliwa na taasisi inayoshughulika na mambo ya utafiti wa kupunguza umasikini (Repoa), ambapo aliitaja sekta ya madini hasa ya dhahabu kuwa ya pili kwa kuliingizia taifa dola bilioni 1.7 kwa mwaka.
Profesa Ndulu, alisema bidhaa za viwandani zimeingiza dola bilioni 1.3 ambayo imepanda baada ya miaka 15 na dola milioni 860 za huduma mbalimbali za mizigo inayosafirishwa kwenda katika nchi jirani.
Mkutano huo wa Repoa uliwakutanisha wadau wa uchumi uliokuwa ukijadili namna ya kuzikabili changamoto na kupata mbinu mbadala za uchumi.
Alisema mabadiliko hayo yamekuwa tofauti na watu wanavyadhania kuwa labda kilimo kingeweza kuongoza katika kuingiza mapato ya fedha za kigeni.
“Watu wengi tunafikiria kuwa mazao ya kilimo ndiyo yanayoingiza fedha nyingi za kigeni, lakini kwa kweli sekta ya kwanza ni utalii, ya pili ni dhahabu ambayo kwa sasa bei ya dhahabu imeshuka katika soko la dunia,” alisema.
Alisema mabadiliko hayo yameifanya sekta ya bidhaa ya viwandani kuwa ya tatu kwa kuingiza dola za Marekani bilioni 1.3 ikiwa ni tofauti kulinganishwa na miaka 15 iliyopita.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kukwama kwa sekta ya kilimo kumetokana na kushindwa kufanyika mapinduzi yenye tija.
Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi anayeheshimika duniani, alisema kama sekta ya kilimo itaongezewa thamani, ni wazi itapunguza gharama ya chakula na kuwafanya wakulima kuwa na hali nzuri ya maisha.
“Unapoongeza thamani pia unaongeza pato la mkulima mkubwa na mdogo, na hili kuwapo uhakika wa mkulima kufanya shughuli zake za kilimo, ni lazima viwanda viwepo,” alisema.
Alisema uwapo wa viwanda ni muhimu kuwa na umeme, miundombinu, na bandari na kupunguza rushwa katika maeneo ambayo ni muhimu katika uchumi wa taifa.
“Vitendo vya kubadili mara kwa mara uongozi bandarini kunadhohofisha ufanisi na kuweka mianya ya rushwa kwa viongozi kujiwekea watu wao na kufanya kila waziri anayepewa madaraka kuweka mtu wake,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alisema mabadiliko ya mfumo imefanya fedha nyingi za kigeni kubaki nje, na ili fedha hizo zibaki ndani ni muhimu Serikali ikaongeza tija katika sekta ya kilimo.
“Utaona hali hiyo inafanya mtu mmoja mmoja kumiliki uchumi, na hata ukiangalia mji wa Arusha ingawa utalii unaongoza, lakini bado upo chini katika uchumi ukilinganisha na Dar es Salaam ambayo imeongoza katika pato la mtu mmoja mmoja, ”alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles