27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wamachinga wavurugwa

machingaNa Waandishi Wetu- Mikoani

WAFANYABIASHARA ndogondogo maarufu kwa jina la wamachinga, wameanza tena kughasiwa licha ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza kuwa wasisumbuliwe na waachwe waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Japo Rais Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo Agosti, mwaka huu katika mikutano yake ya hadhara aliyoifanya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa alipokwenda kujitambulisha baada ya kuchaguliwa Julai 23, mwaka huu kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, lakini wamachinga wataanza kuondolewa katika maeneo wanayofanyia biashara yanayodaiwa kuwa si rasmi.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa walidai kuwa Rais Dk. Magufuli alitoa agizo hilo ili kuwapoza wamachinga kwa kuwa joto la operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) iliyoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lilikuwa limepanda.

Wachambuzi hao walienda mbali zaidi kwa kudai kuwa kama Rais Magufuli asingetoa agizo hilo inadaiwa pengine wamachinga hao wangeandamana katika operesheni hiyo iliyopangwa kufanyika Septemba mosi, mwaka huu kutokana na kile viongozi wa Chadema walichodai kuwa ni kuongezeka kwa matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia lakini haikufanyika kama ilivyopangwa baada ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kutangaza kuiahirisha kwa madai kuwa waliombwa na viongozi wa dini kufanya hivyo ili kulinda amani ya nchi.

Baada ya Rais Magufuli kutoa agizo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ndiye aliyeanza kuibuka na kutaka waondolewe katika maeneo hayo kwa kile alichodai kuwa ni kutokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dar es Salaam kupoteza mapato ya zaidi ya Sh bilioni 100 kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wasio waaminifu wanakwepa kodi kwa kuwapa bidhaa wamachinga ili kuziuza barabarani.

Makonda alitoa agizo hilo Dar es Salaam juzi alipozungumza na waandishi wa habari kwa kutoa siku 14 kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanawaondoa wamachinga hao na kuwarudisha katika maeneo maalumu waliyotengewa kufanya biashara zao ikiwa ni tofauti na alivyoagiza Rais Magufuli.

Siku moja baada ya Makonda kutoa agizo hilo, baadhi ya wamachinga walionukuliwa na vyombo vya habari walidai kuwa hawataondoka katika maeneo hayo hata kama watapigwa mabomu ya machozi kwa kuwa ndiko ambako bidhaa zao zinanuliwa zaidi na wateja wao kuliko maeneo mengine waliyotengewa na Serikali.

Gazeti hili lilipomtafuta Makonda jana kwa njia ya simu ya mkononi ili kupata kauli yake kutokana na msimamo uliowekwa na wamachinga hao, alisema yeye hana utaratibu wa kutoa kauli kwa njia ya simu.

“Kwa hiyo unataka mimi nizungumze kauli yangu kutokea kwako kwa njia ya simu, sidhani….mimi sina utaratibu wa kuzungumza kwa staili hiyo,” alisema Makonda na kumkatia simu mwandishi wa habari aliyempigia.

MWANZA

Kutoka Mwanza, mwandishi wetu, Peter Fabian, anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa muda wa miezi mitatu uliotolewa na Rais Magufuli kwa wamachinga hao kuendelea kufanya biashara zao katika ya jiji unamalizika Novemba 11, mwaka huu.

Mongella alisema wafanyabiashara wataendelea kuwapo katika maeneo hayo hadi muda utakapomalizika na watakutana na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela na kuangalia namna watakayoona inafaa.

“Muda uliotolewa na Rais unamalizika Novemba 11, mwaka huu ukifikia kuna mambo ambayo tutakutana kujadiliana na kuona namna ya kufanya na hiyo tutawataarifu kwa sasa naomba nisiongee chochote,” alisema Mongella.

ARUSHA

Kutoka Arusha, waandishi wetu, Eliya Mbonea na Abraham Gwandu, wanaripoti kuwa Wilaya ya Arusha itaanza kuwaondoa kwa nguvu wamachinga waliozagaa katika mitaa mbalimbali na wengine wakifunga barabara za jiji. Hatua ya kuwaondoa wamachinga hao imefikiwa baada ya kuajiri askari mgambo wapya ambao mikataba yao inatarajiwa kuanza mwezi ujao.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro, alisema mpango wa kuwaondoa wamachinga utaanza kutekelezwa Novemba mosi, mwaka huu.

“Tupo tayari kuwaondoa baada ya kuandaa mazingira ya kufanikisha mpango huu, kulikuwa na sababu kadhaa zilizochelewesha ikiwamo kumalizika kwa mikataba ya askari mgambo ambao wamekuwa wakisimamia utekelezaji wa mpango huo kwa kuusimamia kwa saa 24.

“Lakini pia tulikuwa na vikao vya makubaliano baina ya Serikali na viongozi wa wafanyabiashara hao ili nao waelewe umuhimu wa usafi na mpangilio wa jiji. Kwa hiyo tumekubaliana, tayari mgambo wa kutosha wameingia mkataba na halmashauri na wataanza kazi Novemba mosi,” alisema Daqarro.

Pia alisema wiki ijayo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo itakaa pamoja na watendaji wa jiji ili kukamilisha utaratibu wa kuwaondoa wafanyabiashara bila ghasia na kama italazimika basi Serikali itatumia vyombo vingine vya dola kutekeleza mpango huo.

“Hatukuwa tumelala, ni suala la utaratibu tu ni kwa namna gani wananchi hawa wataendelea kuendesha shughuli zao za maisha huku wakiamini Serikali yao inawajali.

“Hatukutaka kukurupuka bila kuandaa eneo la kuwapeleka, kwa hiyo kama kuna ambao wanadhani si lazima kusubiri mpango huo basi wanaweza kurudi katika maeneo yao ya awali,” alisema Daqarro.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia, alisema tayari wameshaunda kamati ya kushirikiana na wamachinga hao kupitia kwa viongozi wao

“Kabla ya kuanza kuwaondoa tayari tumeshakaa nao kwa zaidi ya vikao vitatu kupitia kwa viongozi wao, tumekubaliana baadhi ya njia tutakuwa tunazifunga jioni ili wao waendeshe biashara. Lakini pia kuna maeneo tutakayowapeleka,” alisema Kihamia.

 

MBEYA

Naye mwandishi wetu, Pendo Fundisha kutoka mkoani Mbeya, anaripoti kuwa Serikali imesema inaendelea na mchakato wa kurekebisha na kuboresha miundombinu ya maeneo yaliyopendekezwa na wamachinga kwa ajili ya kufanyia biashara zao.

Akizungumza mjini hapa juzi na watendaji wa kata na mitaa wa halmashauri, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, alisema katika kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo suala la usafi wa mazingira pamoja na upangaji wa maeneo, tayari wamachinga wametengewa maeneo yao.

Alisema Mbeya ni miongoni mwa majiji ambayo uchumi wake unakua kwa haraka hivyo shughuli za kibanadamu na uzalishaji wa taka unaongezeka kwa kasi kubwa hivyo ni vema wamachinga wakatafutiwa maeneo mbadala.

“Mikakati ya Serikali ni kuhakikisha wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao bila ya kubughuziwa, hivyo mkoa umejipanga kwa kuwa maeneo yapo kilichobakia ni kuboreshwa kwa miundombinu kama ile ya maji, umeme na matundu ya vyoo,” alisema Makalla.

SIMBACHAWENE

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisisitiza umuhimu wa wamachinga kuacha kufanya shughuli hizo katika maeneo yasiyo rasmi hasa kingo za barabara ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaozitumia.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, alisema wamachinga wanapaswa kufuata taratibu kwa kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyotengwa na si vinginevyo.

“Watu wametafsiri vibaya kauli ya Rais Magufuli, aliposema wamachinga wasibughuziwe, si maana yake waachwe hata kama wakivunja sheria, alimaanisha wawekewe utaratibu mzuri wa kufanya biashara, si kuziba barabara, wakuu wa mikoa wanaotoa matamko wanajua walishawatengea maeneo lakini wao hawataki kwenda wanasingizia hakuna biashara wakati wateja wapo,” alisema.

Simbachawene alisema Serikali haikatazi watu kufanya biashara, lakini wamachinga wamekuwa wakiacha maeneo waliyotengewa na kupanga biashara zao barabarani kwa makusudi jambo linalosababisha usumbufu kwa wananchi.

“Tunapaswa kutafsiri hili suala kwa misingi ya haki na uwajibikaji, wajibu wa wakuu wa mikoa ni nini, wamachinga wajibu wao ni nini je, hayo matamko yanaenda kinyume na hivyo vitu, mimi nilidhani labda wamachinga watalalamikia miundombinu ya maeneo husika, mnapaswa kufahamu hali ni mbaya kwa sasa, hakuna mtu hajui adha na matatizo ya wamachinga katika majiji,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles