25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yawashambulia Lowassa, Zitto Kabwe  

edward-lowassa-na-zitto-kabweNa AGATHA CHARLES

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewashambulia wanasiasa wawili wa vyama vya upinzani, Edward Lowassa na Zitto Kabwe, kutokana na msimamo wao wa kuukosoa utawala wa Rais Dk. John Magufuli.

Kauli hiyo ya CCM imekuja baada ya mapema wiki hii, Lowassa ambaye alipata kuwa Waziri Mkuu na baadaye mwaka 2015 kupambana na Magufuli katika Uchaguzi Mkuu akiwania nafasi ya urais kupitia Chadema, kuuchambua mwaka mmoja wa utawala wa kiongozi huyo.

Katika uchambuzi wake Lowassa alisema kuna mafanikio machache katika baadhi ya maeneo, lakini maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu huku akimshutumu Rais Magufuli kwa kuminya demokrasia na kuigeuza kada ya utumishi wa umma kuwa kaa la moto.

Kwa upande wake Zitto amekuwa akiukosoa utawala wa Rais Magufuli na mara kadhaa akimwita dikteta mamboleo.

Jana CCM iliitisha mkutano na waandishi wa habari ambao ulionekana kulenga kujibu mashambulizi dhidi ya wanasiasa hao.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Ofisi za Makao Makuu ya CCM yaliyopo Lumumba, jijini Dar es Salaam, Msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka, alianza kwa kusema kumekuwa na upotoshaji wa taarifa dhidi ya Serikali ya Rais Magufuli zinazotolewa na viongozi wa vyama vya siasa.

Miongoni mwa taarifa hizo kwa mujibu wa Ole Sendeka, ni pamoja na tathmini aliyoitoa Lowassa kuhusu mwaka mmoja wa utawala wa Rais Magufuli.

Ole Sendeka alimpinga Lowassa kuhusu suala la watumishi wa umma, demokrasia na dhana nzima kuhusu mabadiliko.

Alisema tofauti na mtazamo wa Lowassa ni kwamba, Rais Dk. Magufuli anapambana kurejesha nidhamu katika sekta hiyo.

Ole Sendeka alikwenda mbali na kumbeza Lowassa hasa kutokana na tathmini yake katika Uchaguzi Mkuu uliopita kwamba ameonyesha demokrasia na kuleta alama, sura na msisimko mpya katika siasa nchini baada ya kuhamia Chadema.

Katika hilo, Ole Sendeka alisema Lowassa hastahili sifa hizo na kwamba ndiye anayepaswa kushutumiwa kwa kukanyaga demokrasia na si Rais Magufuli.

“Kitendo cha yeye kuhama ghafla na kuingia kwenye chama kimoja asubuhi, mchana kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho anaona kuwa ni demokrasia?

“Haiwezekani utoke ukaharibu demokrasia ya chama kingine kwa ushawishi na sababu ambazo wanajua wenyewe, wanakuteua ambaye hujakitumikia chama hicho wala kukitetea popote na ulikuwa ukikishughulikia kama wengine halafu unakuwa ni alama ya chama hicho. Hujiulizi na unaona fahari hata baada ya mwaka mmoja,” alihoji Ole Sendeka.

Msemaji huyo wa CCM alihoji demokrasia ambayo Lowassa ameifundisha nchi hii na kutaka wataalamu kufanya utafiti ili kufahamu demokrasia iliyotumiwa na Chadema.

Kuhusu watumishi wa umma, Ole Sendeka alisema anashangaa Lowassa kusema umegeuzwa kaa la moto wakati Serikali inawachukulia hatua watumishi walioshirikiana na wakwepa kodi.

Ole Sendeka alisema kama hilo la watumishi ameliita kaa la moto basi la uanzishwaji wa mahakama ya mafisadi atauita moto wa Jehanamu.

Kuhusu mabadiliko Msemaji huyo wa CCM, alisema kila chama cha siasa kilijinadi kuwa kitayaleta baada ya kuchaguliwa.

“Alipoingia Dk. Magufuli kuna watu walizoea kukwepa kodi na kutengeneza faida, unapowazuia na kuwataka walipe kodi athari yake ni kwamba watakuwa na mapato kidogo, watakasirika lakini kwasababu jambo walilokuwa wakilifanya ni ovu hawana ujasiri wa kusimama hadharani na kuisema Serikali hii kuwa inatulazimisha kulipa kodi halali badala yake baadhi yao wametubu na kuanza kufuata kanuni za ulipaji kodi,” alisema Ole Sendeka.

AMSHAMBULIA ZITTO

Kuhusu hatua ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) kuukosoa utawala wa Rais Magufuli, Msemaji huyo wa CCM alisema imetokana na Serikali ya awamu ya tano kuwashughulikia maswahiba wake.

Ole Sendeka alimshutumu Zitto kwa kutumia nafasi aliyokuwa akiishikilia katika Bunge la 10 ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) kuwalinda wale aliowaita maswahiba zake.

Alidai kuwa Uenyekiti wa Zitto PAC ulikuwa ni kichaka cha kuficha madudu ya baadhi ya wakubwa wa mashirika ya umma ambao ni marafiki zake.

Pasipo kulitaja jina, lakini maelezo yake yalionekana kulilenga Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ole Sendeka alisema ni miongoni mwa taasisi iliyokumbwa na madudu ambayo alikuwa anasimamia rafiki yake Zitto.

“Baadhi ya marafiki zake ndio hao wamenunua hekari moja kwa milioni 800, kumbe walikuwa wanajificha, nyuma ya pazia kulikuwa na masilahi binafsi na wakati umefika wa Serikali si tu kuwashughulikia viongozi wa taasisi hizo bali hata kuangalia akaunti za viongozi wa kamati za Bunge waliokuwa wakisimamia mashirika haya ambayo yameonesha ufisadi mkubwa,” alisema Ole Sendeka.

 

VYOMBO VYA HABARI

Wakati huo huo, Ole Sendeka alidai kuwapo kwa magazeti mawili ya kila wiki ya hapa nchini na mengine mawili ya nje ya nchi yanayotumika na watu aliowataja kuwa na ukwasi mkubwa kuipaka matope Serikali.

Ole Sendeka alikataa kuyataja magazeti hayo lakini alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa jarida moja la nje ya nchi linalotumika ni lile la The Economist la nchini Uingereza.

Alisema jarida hilo pamoja na magazeti hayo yanaandika habari ambazo kimsingi zinakejeli, kudhihaki, kukatisha tamaa, kubeza, kuchafua na kudhoofisha jitihada zinazofanywa na Serikali.

Hata hivyo, alisema wao kama chama tawala hawajali kukosolewa maana wao ni waumini wa kukosolewa na dhana ya kujikosoa na kujisahihisha.

ADAI CHAMA CHAMWAGIWA FEDHA

Katika hatua nyingine, Ole Sendeka alisema wamepata taarifa za kigogo mmoja wa vyama vya upinzani anayedaiwa kupewa kiasi cha dola milioni 15 zitakazomsaidia kupanga safu yake ya uongozi.

Alikitaja chama hicho kuwa ni kile kinachotarajia kufanya uchaguzi wake mwakani na kwamba fedha hizo zitatumika kuwavuruga.

Alisema viongozi wake wakiwamo wale wa kutoka Zanzibar, wamekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles