Na Ramadhan Libenanga, Morogoro
AGIZO la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Theresia Mahongo kupiga marufuku wafanyabiashara wa Soko la Mitumba la Sabasaba, jana liligonga mwamba baada ya wafanyabiashara hao kuwagomea askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
MTANZANIA liliwashuhudia wafanyabaishara hao wakiendelea kupanga biashara zao barabarani bila kujali askari na mgambo wa manispaa waliokuwa wamevalia sare zao.
Askari hao walipoona hali hiyo, waliamua kuondoka baada ya wafanyabiashara hao kuanza kujikusanya kutaka kuvamia gari la manispaa lililokuwa limebeba FFU na mgambo.
Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wafanyabiashara walisema waliamua kuwagomea askari hao kutokana uongozi huo wa manispaa kuwazuia kufanyabiashara kando kando ya barabara huku ikiwaruhusu baadhi yao.
“Tunashangazwa na uongozi kutuzuia sisi huku Sabasaba, lakini wanaacha wafanyabiashara kule mjini eneo la Islam ambako ni mjini kabisa,“ alisema Jalala Uweso, mmoja wa wafanyabiashara wa mitumba.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao wameiomba manispaa kuwaandalia eneo lenye miundombinu muhimu na inayofikiwa na wateja kwa urahisi kabla ya kuwafukuza katika eneo hilo ambalo lina wateja wa kutosha.