ELIZABETH HOMBO Na SARAH MOSES-DAR/DODOMA
RAIS Dk. John Magufuli amesema Kampuni ya mawasiliano ya Airtel ni mali ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Kutokana na hilo, amemwagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kufuatilia kwa karibu umiliki wa kampuni hiyo kabla mwaka huu kumalizika.
Mkuu huyo wa nchi, alitoa kauli hiyo jana katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inayojengwa eneo la Makulu mjini Dodoma.
“Waziri wa Fedha, hakikisha unafuatilia suala la Airtel. Kwa taarifa nilizonazo Airtel ni mali ya TTCL, kuna michezo michafu imefanyika, sasa sitaki kuzungumza mengi, fuatilia hilo, nchi ilikuwa na maajabu kweli.
“Unachukua share leo, kesho inauzwa… zinafutwa halafu zinauzwa kwa dola moja, maajabu kweli, hakikisha huo mchezo unamalizika kabla ya mwaka huu kuisha, kwa namna hiyo lazima vyuma vitabana tu,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Serikali, kilisema kuwa katika uchunguzi huo wote waliohusika katika mpango huo watachukuliwa hatua, ikiwamo kufikishwa mahakamani.
HISTORIA YA TTCL/AIRTEL
Mwaka 1998, TTCL ilianzisha kampuni tanzu ya Cellnet ambayo ilifanya kazi hadi mwaka 2001, ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel Tanzania, huku umiliki wake ukiendelea kuwa chini ya shirika hilo kwa asilimia zote baada ya kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 11.
Pamoja na hilo, Januari 31 mwaka 2002, Celtel ikiwa chini ya umiliki wa TTCL, ilikopa Sh bilioni 180.4 ili kukuza mtaji wake.
Wakati huo, TTCL ikiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 600 sawa na Sh trilioni 1.32, ilikuwa inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi.
Katika hilo, Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 65 ya hisa zote na mbia huyo asilimia 35 zilizosalia.
Mwaka 2005, mabadiliko yalifanywa katika Bodi ya Wakurugenzi ya Celtel kwa lengo la kuunda kampuni mbili tofauti; Celtel ikitenganishwa na TTCL.
Hata hivyo, kutokana na mabadiliko hayo, Celtel iliwekwa chini ya umiliki wa MSI ambayo Septemba 2007 iliuza hisa zake kwa Kampuni ya Zain, ambayo nayo ilikuja kuziuza kwa Bharti Airtel, Juni 8, 2010.
Inadaiwa kuwa uwekezaji wa TTCL ilioufanya Celtel na baadaye Airtel, ambayo thamani yake imeongezeka zaidi, haulingani na inachokipata.
Madai hayo yanatokana na namna umiliki wa hisa ulivyobadilishwa baada ya Celtel kutenganishwa na TTCL ambayo ilipewa hisa chache tofauti na inavyostahili.
Kwa sasa, Airtel Tanzania inamilikiwa na Serikali yenye asilimia 40 na Celtel Tanzania BV, kampuni tanzu ya Zain Africa BV ambayo ilinunuliwa na Bharti Airtel International, Novemba, 2010 ikiwa na asilimia 60.
Hivi karibuni yalifanywa mabadiliko na Serikali iliilipa Bharti Airtel Sh bilioni 14.7 na kuchukua asilimia 35 ya hisa ilizokuwa inamiliki na kuifanya imiliki asilimia zote za TTCL.
Sheria mpya iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge imeibadili TTCL inayohudumia asilimia 0.82 ya soko kuwa shirika la umma la mawasiliano na kulipa jukumu kubwa katika sekta ya mawasiliano nchini.
Bharti Airtel inatakiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kukidhi vigezo vya Sheria ya Posta na Mawasiliano ya mwaka 2010, lakini bado haijafanya hivyo.
JPM AIPA RUNGU NBS
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli pia aliitaka Ofisi ya Taifa ya Takiwmu (NBS), pamoja na vyombo vingine husika, kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote ama taasisi itakayotoa takwimu za upotoshaji.
Alisema NBS ina wajibu wa kuendelea kutoa taarifa kwa weledi, huku akitoa onyo kwa watu wanaotoa taarifa za kitakwimu za nchi ambazo hazijatolewa wala kuthibitishwa na taasisi hiyo.
“Mtu au shirika akitoa takwimu za upotoshaji tofauti na za kwenu, Dk. Chuwa wewe mkamate weka mahabusu akajifunze kuandikia takwimu huko wakati akisubiri kwenda mahakamani. Na sheria ya takwimu kifungu cha sheria namba 37 imeeleza adhabu za kosa hilo kuwa ni kifungo cha miezi mitatu hadi miaka sita jela, faini isiyopungua Sh milioni mbili au vyote kwa pamoja.
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania tumieni takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, puuzeni takwimu za kupika zinazotolewa na baadhi ya watu kwenye mitandao, wapuuzeni hata wanaosema vyuma vimebana, vyuma vimebana kwa wanaotaka vya bure, lakini wanaochapa kazi vyuma havijabana.
Rais Magufuli alisema vyuma vitaendelea kukaza kwa watu ambao walikuwa wamezoea kupata fedha za bure, lakini kwa wanaofanya kazi halali vimeachia na ataendelea kubana hao wachache ili kuachia kwa Watanzania walio wengi.
“Hata wanaosema vyuma vimebana wakati ninyi watu wa takwimu mnasema vimeachia, wakamateni wawaeleze vimekaza wapi,” alisema Rais Magufuli…..
Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya MTANZANIA