25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

UCHUNGUZI WA TUNDU LISSU, SAANANE, AZORY BADO MBICHI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


JESHI la Polisi nchini limezungumzia matukio ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, pamoja na kupotea kwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Ben Saanane na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi mkoani Pwani, Azory Gwanda (42).

Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, alisema uchunguzi wa matukio hayo bado unaendelea.

“Suala la Lissu limezungumzwa sana na viongozi, jeshi linachukulia tukio hilo ‘serious’, tumechukua hatua zote zitakazotuwezesha kujua nani alitenda tukio hilo,” alisema Boaz.

Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7 mwaka huu akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma ambako alikuwa akitekeleza majukumu yake ya kibunge.

Hadi sasa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumzia tukio la kupotea kwa Saanane, alisema pia upelelezi bado unaendelea.

“Hatuwezi kusema kila hatua tunayochukua, hairuhusiwi kisheria na hata katika kanuni zetu za upelelezi…tunaomba wenye taarifa zaidi watuletee,” alisema.

Saanane alipotea tangu mwaka jana katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa hajulikani alipo jambo ambalo limezua hofu kama yu hai ama la.

Alisema jeshi hilo pia limepokea taarifa za kupotea kwa Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi mkoani Pwani na kwamba uchunguzi unaendelea.

Gwanda alitoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 21, mwaka huu, akiwa katika kituo chake cha kazi Kibiti mkoani Pwani na hadi sasa hajapatikana.

“Tumepokea taarifa ya mwandishi kupotea, tunachukua kila hatua inayostahili. Ziko taratibu ambazo tunapaswa kuzichukua kama polisi hivyo tuwe na subira,” alisema.

Katika hatua nyingine jeshi hilo limesema upelelezi dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye anakabiliwa na tuhuma za uchochezi bado unaendelea.

“Tunaendelea na uchunguzi kwa sababu kuna vitu vilikuwa vina – miss, ili mtu ashtakiwe lazima vigezo vinavyotengeneza kosa vipatikane, viki – miss maana yake hatuwezi kwenda mbele zaidi ya hapo,” alisema Boaz.

MATUKIO YA UBAKAJI

Jeshi hilo limesema matukio ya ubakaji, ulawiti na kunajisi watoto wadogo yameongezeka kwa kiwango kikubwa.

Katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2017 matukio yanayohusisha kubaka, kulawiti, kunajisi, mauaji, kutupa watoto na usafirishaji binadamu yameripotiwa 11,620 ukilinganisha na matukio 11,513 yaliyoripotiwa mwaka jana.

Boaz alisema makosa ya ubakaji yaliyoripotiwa mwaka huu ni 7,460 ukilinganisha na makosa 6,985 yaliyoripotiwa mwaka jana wakati makosa ya kunajisi ni 25 ukilinganisha na 16 yaliyoripotiwa mwaka jana.

“Makosa haya ni mengi kuliko mengine yoyote na sababu kubwa zinazochangia ni mmomonyoko wa maadili, ushirikina na tamaa za mwili.

“Tiba yake iko kwenye jamii na sisi tutaweka msisitizo mwakani ili toune tumefikia hatua gani,” alisema Boaz.

Alisema makosa mengine kama ya unyang’anyi wa kutumia silaha, uhalifu wa kifedha, makosa ya maadili ya jamii na yale ya usalama barabarani yamepungua ukilinganisha na mwaka jana.

Alifafanua kuwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi wa magari, pikipiki na mifugo mwaka huu yameripotiwa 29,677 wakati mwaka jana yalikuwa 34,830…….

Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya MTANZANIA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles