Na Elias Msuya
ILE safari ya zaidi ya kilometa 1,200 ya makada watatu wa Chadema kutoka mkoani Geita waliotaka kwenda Ikulu ya Dar es Salaam kumwona Rais Jakaya Kikwete, imeishia mikononi mwa polisi baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, kuwazuia kuendelea na safari yao hadi watakapopata maelekezo.
Vijana hao, Khalid Selemani, Athanas Michael na Juma Maganga, walisema wameamua kutembea kwa miguu kwa siku 37 ili kumfikishia Rais Kikwete ujumbe wao kuhusu kupinga ufisadi, kudai nchi ya Tanganyika, kuhimiza umoja na uzalendo, haki za binadamu na kupinga umaskini.
Huku wakionekana kuchoka na safari hiyo baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam jana, vijana hao waliokuwa wamevalia majoho ya magunia na kujifunga bendera ya Tanzania huku wameshikilia bendera za Tanganyika, walikuwa wakisindikizwa na makada wengine wa Chadema waliovalia magwanda ya khaki.
Walipofika Ubungo kwenye taa za kuongoza barabara, walikutana na askari wa Jeshi la Polisi waliowasimamisha na kuanza kuwahoji, kisha wakaanza kuongoza maandamano yao kwa magari mawili aina ya Baloon na Land Cruiser iliyokuwa imejaza askari.
Wafika kwa DC Kinondoni
Walipofika Magomeni kwenye taa za kuongozea barabara, ndoto yao ya kumwona rais ikayeyuka baada ya polisi waliokuwa wakiwaongoza kuwataka kwanza kuingia kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
Baada ya kufanya mazungumzo na mkuu wa wilaya, Rugimbana kwa karibu saa nzima, vijana hao walitolewa nje.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano na vijana hao, Rugimbana alisema wamevunja sheria kwa kuandamana bila kuwa na kibali.
“Kama kweli hawa vijana wametembea nchi nzima kwa miguu bila idhini, basi wamevunja sheria. Walipaswa kuwa na kibali cha kwenda Ikulu,” alisema Rugimbana.
“Kama ni kwenda Ikulu kumwona rais ni ruhusa, lakini hayo matembezi yao kwa leo yataishia hapa. Taarifa nitaifikisha Ikulu. Rais anaweza kuagiza wasaidizi wake wawaone au yeye mwenyewe awaone,” aliongeza.
Waapa kufika Ikulu
Baada ya tamko la Rugimbana, vijana hao waliruhusiwa kuondoka katika ofisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi wa msafara huo, Khalid Selemani alisema wao walikuwa wanaazimia kuendelea na matembezi yao.
“Naomba nitoe kilio chetu, tumetembea kwa siku 37 halafu tunaambiwa tuishie hapa. Tunaamini kwamba haya matembezi yetu hayahitaji kibali,” alisema Selemani.
Baada ya kutoa matamko yao walianza kwenda Ikulu kama walivyodai. Hata hivyo, polisi waliokuwapo eneo hilo waliwakamata na kuwapeleka katika Kituo cha Polisi cha Magomeni.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mwenyekiti wa Bavicha Kata ya Kwembe, Isaya Msabila aliyekuwa akiwasindikiza vijana hao, alisema awali vijana hao waliopanga matembezi hayo walikuwa 200 lakini walioanza safari kutoka Geita walikuwa saba na wanne kati yao waliishia njiani, hivyo wakabaki watatu.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema baada ya vijana hao kukamatwa, chama kilituma vijana wengine kuwawekea dhamana lakini nao walikamatwa.