27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

WALIOSAINI MKATABA MLIMANI CITY KIKAANGONI

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imebaini madudu katika mkataba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye mradi wa Mlimani City na kuagiza waliohusika kusaini waitwe kuhojiwa.

PAC pia imeagiza deni analodaiwa mwekezaji huyo (Mlimani Holdings) lihakikiwe upya na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na lilipwe kabla ya Juni 30.

Maagizo hayo yalitolewa na kamati hiyo jana baada ya kutembelea baadhi ya maeneo ya mradi huo na kueleza kuwa haijaridhishwa na utekelezaji wake tangu mkataba ulipoingiwa mwaka 2004.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka (Chadema), alisema mkataba huo una upungufu mkubwa unaoacha maswali mengi na huenda kuna vitu vimejificha.

“Mkataba huu ni mbovu sana na una mapungufu na ili haki itendeke, tunaagiza wahusika wote waliouandaa mwaka 2004 waje mbele ya kamati watoe maelezo kwanini walisaini mkataba mbovu kama huu.

“Kuna vitu vingi vimejificha tutajua hatua gani zichukuliwe, lakini ni lazima watu wawajibishwe,” alisema Kaboyoka.

WALIOINGIA MKATABA

Taarifa zinaonyesha walioingia mkataba huo ni aliyekuwa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Mathew Luhanga na aliyekuwa Ofisa Utawala Mkuu wa chuo hicho, Profesa John Mshana.

Waliingia mkataba huo Juni 5 mwaka 2004 na wawekezaji (Mlimani Holdings) ambao ni Gulaam Abdoola na Rizwan Desai.

MAENEO YENYE UTATA

Kamati ilibaini mradi wa ujenzi wa hoteli ya nyota tatu ambayo itakuwa na vyumba 100 na bustani ya mimea na wanyama, bado haujaanza wakati mkataba unaonyesha inatakiwa ikamilike mwakani.

Alisema awali uongozi wa chuo ulivyoitwa bungeni, walisema mwekezaji amekataa kujenga hoteli hiyo, lakini jana walisema hoteli itajengwa.

“Kwa miaka 12 haikujengwa halafu iwezekane kwa mwaka mmoja uliobaki? Tunaagiza tuletewe mpango wa utekelezaji wa mradi mzima ambao unaonyesha ni lini itaanza kujengwa hadi kukamilika kwake,” alisema Kaboyoka.

Mtaji wa Sh 150,000

Pia katika taarifa yake, uongozi huo wa chuo uliiambia kamati hiyo kuwa mwekezaji huyo alikuja na mtaji wa dola za Marekani 75 (takribani Sh 150,000) huku akisema fedha nyingine za kuendesha mradi huo ni mkopo.

Kutokana na maelezo hayo, Mbunge wa Viti Maalumu, Hadija Nassir (CCM), alihoji: “Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni taasisi kubwa inayoheshimika ndani na nje ya nchi, hatukutegemea kukuta madudu kama haya.

“Hivi kweli mlishindwa kukopa fedha kuendesha mradi huu hadi mkubali mwekezaji wa aina hii?”

Eneo jingine lenye utata ni lile la kupunguzwa muda wa mkataba kutoka miaka 50 hadi 35 na kulipwa kwa kodi ya pango kwa ardhi ambayo mwekezaji hataiendeleza.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Ruge (Chadema) alisema: “Tumeambiwa ukubwa wa eneo hapa ni mita za mraba 44,000, mimi si mtaalamu, lakini kwa macho ya kawaida sidhani kama mita zinazotajwa zimefikia.”

MALIPO PUNGUFU

Kamati ilibaini kuna ukiukwaji mkubwa wa malipo ambayo mwekezaji anatakiwa kukilipa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mkataba unaonyesha chuo hicho kinapaswa kipate asilimia 10 ya mapato ya kodi ghafi, lakini mwekezaji hulipa baada ya kutoa gharama za uendeshaji badala ya kuzijumuisha.

“Uhakiki uliofanywa na wataalamu unaonyesha deni lililotajwa si sahihi, hivyo tunaagiza lihakikiwe upya na CAG apelekewe taarifa kujiridhisha na lilipwe kabla ya Juni 30, mwaka huu,” alisema Mwenyekiti wa PAC, Kaboyoka.

Awali Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo na Uwekezaji wa chuo hicho, Dk. Pancras Bujulu, alisema hadi kufikia Februari mwaka jana, chuo kinamdai mwekezaji huyo Dola za Marekani 304,103.46.

Alifafanua kuwa kuanzia mwaka 2007 hadi 2017, malipo yaliyolipwa na mwekezaji huyo kutokana na pango ni Sh bilioni 16.7 (wastani wa Sh bilioni 1.5 kwa mwaka).

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Utawala, Profesa David Mfinanga, alisema tayari wameunda kamati kupitia upya mkataba huo.

“Hatujakubaliana na hali hii ndiyo maana tuko kwenye mgogoro, tumeshawapelekea madeni wanayotakiwa kulipa, lakini mwanasheria wao mara ya mwisho alituandikia barua kukataa kulipa,” alisema Profesa Mfinanga.

UONGOZI WAKIRI UPUNGUFU

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, alikiri kuwa mkataba huo una matatizo, hivyo watachukua hatua kuyatatua.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Profesa James Mdoe, alisema mkataba huo una upungufu mkubwa unaohitaji kufanyiwa kazi na kwamba watahakikisha menejimenti ya chuo hicho inaufanyia kazi.

MLIMANI HOLDINGS

Taarifa zinaonyesha mwekezaji (Mlimali Holdings) alitaka kuongezwa jina la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili mikutano na shughuli za Serikali zifanyike katika kumbi zake, lakini chuo kilikataa.

Mwekezaji huyo pia alikataa kupunguza muda wa mkataba kwa kile alichodai kuwa mkopo wa fedha za kuendesha mradi huo umejikita katika kipindi cha mkataba mzima.

Pia walikataa kulipa kodi ya ardhi ambayo haijaendelezwa kwa kigezo kuwa mkataba unawaelekeza kuirejesha kama hawataiendeleza.

Hata hivyo, Meneja Mkuu wa Mlimani City, Pastory Mroso, aliihakikishia kamati hiyo kuwa hadi kufikia mwakani hoteli itakuwa imejengwa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Je waliosaini mikataba mibovu ya madini vipi. Hukumu tofauti ni nani kasababisha hasara kubwa.Wakaangni waliosaini mikataba mibovu madini na walioshindwa kusimamia mali za umma wakiwa madarakani na acheni double standard.Rekebisheni sheria mbovu ili watu waache kuchezea nchi. Msichague huyu aende na mwingine asiende. Wate wameliletea hasara Taifa na acheni kuimba kila siku.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles