24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DPP ARUDISHA TAKUKURU JALADA LA ALIYEKUWA MHASIBU WA TAASISI HIYO

Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM 

JALADA la kesi ya aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na wenzake watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya kumiliki mali nyingi zisizo na maelezo, kughushi na kutakatisha fedha, limerudishwa Takukuru kwa upelelezi zaidi.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.

Wankyo alidai jalada la kesi hiyo lilikuwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini kwa kusomwa na limesharudishwa Takukuru kwa upelelezi zaidi.

“Takukuru watakapokamilisha watarejesha tena jalada kwa DPP ili kujiridhisha kama maelekezo aliyotoa yametekelezwa,” alidai Wankyo.

Naye Wakili wa utetezi, Alex Mshumbusi, alidai hategemei kuona upelelezi unachukua muda mrefu kwa sababu mshtakiwa Gugai alikuwa mtumishi wa taasisi hiyo.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hadi Januari 31, mwaka huu kwa kutajwa.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.

Walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba mwaka jana wakikabiliwa na jumla ya mashtaka 43.

Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa Gugai anadaiwa kati ya Januari 2005 na Desemba 2015 akiwa ofisa wa umma aliyeajiriwa na Takukuru, anamiliki mali zenye thamani ya Sh 3,634,961,105.02 ambayo haiendani na kipato chake cha sasa na cha nyuma ambacho ni Sh 852,183,160.

Alidai shtaka la pili hadi la sita, Gugai anadaiwa kughushi mikataba ya mauziano ya nyumba akionyesha kauza kwa watu mbalimbali wakiwamo washtakiwa wenzake, hivyo walionunua ndio wamiliki halali wakati si kweli.

Anadaiwa kuonyesha kuwa Agosti,2007 alimuuzia Zenna Mgallah plot namba 225 block 6, iliyopo Mbweni JKT,  Julai 2011 alionyesha kauza nyumba namba 621,622 na 623 zilizopo block A Gomba Arumeru kwa Salehe Saa wakati si kweli.

Gugai anadaiwa Oktoba 20,2013 kwa kughushi alionyesha kamuuzia Arif Premji nyumba namba 64 iliyopo Ununio, Desemba 20, 2014 alionyesha kamuuzia nyumba namba 737 block C Edith Mbatia iliyopo Mwarongo, Tanga na shtaka la sita anadaiwa alidanganya kuonyesha kamuuzia Mbatia nyumba namba 1, 2, 3 block J iliyopo Mwarongo.

Shtaka la saba linamkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili, Makaranga ambao inadaiwa Novemba 20, 2011 walighushi mkataba kuonyesha Gugai kamuuzia Makaranga nyumba namba 150 block 8 iliyopo Bunju akionyesha ndiye mmiliki.

Shtaka la 8 hadi la 11 la kughushi pia linamkabili mshtakiwa wa kwanza na wa tatu, Aloys ambao inadaiwa Novemba 19, 2009 Gugai alionyesha kamuuzia Aloys nyumba namba 275, 277, 296 na 297 zilizopo block 2  Nyamhongolo, Mwanza.

Shtaka la tisa, Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia Aloys nyumba namba 90 block 5 Bugarika Mwanza, shtaka la kumi kamuuzia Aloys nyumba namba 713 block B Kiseke, Mwanza na Oktoba 20, 2015 alionyesha kamuuzia nyumba nyingine namba 230 block B Nyegezi, Mwanza.

“Mheshimiwa hakimu, shtaka la 12 mpaka 20 linamkabili mshtakiwa wa kwanza Gugai ambaye anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia nyumba Manwal Masalakulangwa Bunju, Bagamoyo na Buyuni Temeke.

“Mshtakiwa anadaiwa kughushi mkataba wa mauzo akionyesha kamuuzia Rose Abdallah nyumba mbili Dodoma, Mwongozo Temeke, Chidachi North na Itege Dodoma.

“Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia nyumba Patrick Magesa nyumba mbili zilizopo mkoani Tanga, huku akionyesha mnunuzi huyo ndiye mmiliki,” alidai Wankyo.

Katika shtaka la 21 na 22 Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia nyumba mbili mshtakiwa Yasini Katera zilizopo Nyegezi, Mwanza na kuonyesha ndiye mmiliki.

Kuanzia shtaka la 23 hadi 43, washtakiwa wanashtakiwa kwa kutakatisha fedha ambapo shtaka la 23 hadi 27, Gugai anadaiwa kuficha umiliki wa mali huku akijua ni mazalia ya mali zisizo na maelezo ambalo ni kosa tangulizi la kutakatisha fedha.

Nyumba hizo ni zile alizodai kuuza kwa Zena, Salehe, Arif, na Edith.

Shtaka la 28 linamkabili Gugai na Makaranga wanaodaiwa kutakatisha fedha kwa kuficha umiliki wa nyuma aliyouza Gugai kwa Makaranga na shtaka la 29 hadi 32 linamkabili Gugai na Aloys.

Gugai anadaiwa kutakatisha fedha kwa kuuza nyumba nne kwa Aloys huku akijua ni zao la mali zisizokuwa na maelezo ambalo ni kosa tangulizi la utakatishaji fedha.

Shtaka la 33 mpaka la 41 linamkabili Gugai ambaye anadaiwa kutakatisha fedha kwa kumuuzia nyumba tatu Masalakulangwa,  nyumba nne Rose na nyumba mbili Patrick huku akijua ni zao la rushwa ambalo ni kosa tangulizi la kutakatisha fedha.

Shtaka la 42 na 43 linawakabili Gugai na Yasini ambapo Gugai anadaiwa kumuuzia nyumba mbili Yasini huku akijua ni mazalia ya rushwa ambalo ni kosa tangulizi la kutakatisha fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles