KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
SERIKALI imewafikisha mahakamani watu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la wizi wa mapipa 20 ya mabaki ya madini yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 900.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Agustino Mbando na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Jenifa Masue.
Jenifa aliwataja washtakiwa kuwa ni Jacob Kihombo, Yahaya Masoud, Mbaraka Lipinda, Ramadhani Zombe, Waziri Kibua, Mustapha Mnyika na Richard SÃ ngana.
Akisoma mashtaka, Jenif alidai washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Februari 6 na 7 mwaka huu ndà ni ya Dar es Salaam.
Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kula njama ya wizi wa mali inayosafilishwa.
Katika shtaka la pili ilidaiwa katika tarehe hizo, washtakiwa wote waliiba mali hiyo ambayo ni mapipa 20 ya mabaki ya madini aina ya Tantalite Concentrates.
Ilidaiwa madini hayo yana thamani ya Sh 938,339,907 mali ya Kampuni ya Bollore Transport and Logistics.
Shtaka la tatu linamkabili Zombe ambaye ni mlinzi akidaiwa katika tarehe hizo akiwa mwajiriwa wa Kampuni ya Bollore, alishindwa kuzuia kutendeka kwa kosa la wizi wa mapipa hayo ya madini.
Washtakiwa wote walikana mashitaka na walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hadi Aprili 9 mwaka huu kesi itakapotajwa tena.