Na ELIYA MBONEA, ARUSHA
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ametangaza msako mkali ikiwamo kuwachukulia hatua za sheria watendaji waliofuja asilimia tano ya fedha zinazotengwa katika bajeti kusaidia vijana na wanawake katika halmashauri.
Akizungumza mjini hapa jana na vijana wajasiriamali na wasanii zaidi ya 200 wanaoendesha shughuli zao jijini hapa, alisema serikali haiko tayari kuona vijana waliopangiwa bajeti ya kusaidia kuendesha shughuli zao wakikwamisha na watu au kikundi cha watu wachache.
Alisema ni dhamira ya serikali kuona kila aina ya rasilimali inayopatikana nchini inawanufaisha wananchi na kuwaletea maendeleo hivyo hapatakiwi kuwapo na sababu yoyote ya kushindwa kufanya hivyo.
“Niwaagize Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha asilimia kubwa ya fedha zinazopatikana zinakwenda kuwasaidia wananchi wa Arusha na si vinginevyo.
“Nitaandaa ratiba ya kutembelea kila kata za Jiji la Arusha kukagua na kujionea hizi fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuwasaidia vijana na wanawake zimetumika inavyotakiwa,” alisema Gambo.