NA FARAJA MASINDE
ALIYEKUWA PWANI
TAASISI ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), inayofundisha Lugha ya Kichina, imetoa zawadi kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini waliofanya vizuri kwenye masomo ya lugha hiyo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi hao iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Baobab iliyopo Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Profesa Zhang Xiaozhen, alisema wanafunzi walioshiriki wamejitahidi kutokana na mafunzo waliyoyapata.
Alisema walimu waliokuwa wanafundisha masomo ya Kichina wamejitahidi na kuhakikisha kwamba mwanafunzi anaelewa kwa kadiri anavyofundisha lugha hiyo, lengo likiwa ni kuzidi kujenga uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China.
“Tulikuwa na walimu wa kutosha ambao waliamua kujitolea kufundisha wanafunzi lugha hiyo na hivyo tunashukuru wanafunzi wamejitahidi kujifunza na kuelewa,” alisema Profesa Zhang.
Alizitaja baadhi ya shule sita zilizoshiriki katika mashindano hayo ya lugha ya Kichina na tamaduni zake, kuwa ni pamoja na Baobao Boys na Girls, St Mathew, King David ya mkoani Mtwara na nyinginezo.
Alisema Taasisi ya Confucius imeandaa zawadi mbalimbali kwa ajili ya washindi hao ambapo ni pamoja na fedha taslimu na cheti ili kutoa hamasa kwa wanafunzi kuzidi kupenda lugha hiyo.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Baobab, Halfan Swai, alisema mwaka huu kumekuwa na mwamko mkubwa wa wanafunzi kujifunza Kichina, ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo wengi walikuwa wanasoma Kifaransa.