KAMPALA, UGANDA
WANANCHI walioathiriwa na mafuriko katika Wilaya ya Butaleja Mashariki mwa Uganda, wameishutumu Serikali kwa kuchelewa kuwapelekea msaada.
Kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo, mamia ya watu wameyaacha makazi yao na bustani zilisombwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa.
Waandishi wa Gazeti la Monitor la Uganda walipotembelea maeneo yaliyoathiriwa, waligundua watu wengi wakiwa kwenye hifadhi ya makazi kwenye shule na makanisa, huku wakilalamika hawajapokea msaada wowote kutoka kwa Serikali tangu Ijumaa.
Mafuriko yalileta athari, hasa kuharibika kwa miundombinu baada ya kupasuka kwa kingo za Mto Manafwa.
Msemaji wa Serikali ya wilaya, alisema kuwa kamati inayoshughulikia majanga bado inatathmini hali ilivyo na madhara yaliyojitokeza.
Mamlaka zinasema kuwa wanafanya mipango ya kufanya tathmini ili kupata idadi kamili ya watu walioathiriwa na mafuriko.
Eneo la Butaleja pekee nyumba 650 ziliathiriwa na mvua, na si mara ya kwanza kupata adha ya aina hiyo.
Serikali ilisema ilitoa tahadhari kwa wakazi walioathirika.