Mwandishi Wetu, Arusha
Walimu walioungana na kuanzisha shule ya sekondari ya Arusha City Boys, wamezindua utaratibu mpya wa wanafunzi wao kuanza kusoma kwa kutumia tableti (kishkwambe) hali ambayo inapunguza matumizi ya madaftari lakini kuwaongezea uelewa wanafunzi kujifunza.
Mkurugenzi wa shule hiyo, mwalimu, Daniel Josiah anasema wameweza kununua tablet kwa wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza na wameanza kuzitumia kusoma hali ambayo imeanza kuongeza ufaulu na ujuzi wa mambo mbalimbali kielimu kwa wanafunzi.
“Mabadiliko ya Sayansi na Technolojia, ambayo yanaendelea duniani yametufanya sisi kama walimu tubuni njia nyingine za kufundisha wanafunzi ili kuwawezesha kuwa na ujuzi na mbinu za kisasa katika matumizi ya TEHAMAkatika elimu,”anasema
Mwalimu Josiah anasema Mpango huu umekuwa na manufaa makubwa kwani sasa, walimu wanaandaa masomo yao na kuwatumia wanafunzi kwenye tablet zao zilizounganishwa na mtandao na kazi yao wanafunzi na kujisomea na kujibu maswali ambayo wanaulizwa kulingana na somo husika.
Mwalimu Nyaonge Masato anasema Shule yetu pia imejiunga na program ya Globalgateway chini ya British Council International ambapo wanafunzi wamejifunza Mada mbalimbali pamoja na kujenga mahusiano na Shule nje ya Nchi “alisema
Anasema programu hiyo inakwenda sambamba na kuimarisha mahusiana na shule kadhaa katika nchi za Marekani,Uingereza na nyingine kwa njia ya Video Conferencing na Skype.
“Katika hizi tablet wanafunzi wanapata masomo tu na tumeziwezesha kutowapa fursa ya kuingia katika tovuti nyingine ambazo sio za masomo,” anasema.
Mwanafunzi, Kassim Haruna, anasema kutumia tablet imekuwa na mafanikio kwani wanapata masomo yote kupitia mtandao kwa urahisi zaidi .
Anasema matumizi ya tablet(kishkwambe) kuna rahisisha hata kujua mifano mbali mbali ya mada ambazo wanajifunza kutoka nchi nyingine na wanataaluma wengine .