30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Walimu wahamasishwa kujiendeleza kielimu

 
Na Veronica Simba, Dodoma
 
Serikali imewahamasisha Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari nchini, kujiendeleza kielimu katika ngazi mbalimbali ili kuboresha zaidi utendaji wao wa kazi.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma leo, Januari 7, 2021 na Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama wakati akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara.

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (katikati), akifafanua masuala mbalimbali kuhusu wajibu na haki za Walimu, katika mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), Dodoma, Januari 7, 2021.

Akifafanua, amesema kuwa, kujiendeleza kielimu ni haki ya msingi kwa watumishi wote wa umma wakiwemo walimu, ndiyo maana Serikali kupitia Tume imekuwa ikiwahamasisha kuitumia fursa hiyo ipasavyo.

Chitama amekemea tabia ya baadhi ya Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania Bara, ambao hukataa kutoa ruhusa kwa watumishi walio chini yao wenye nia ya kujiendeleza kielimu.

Hata hivyo, Kaimu Katibu huyo amesisitiza kuwa Walimu wote wa shule za umma wenye nia ya kujiendeleza kielimu, wanapaswa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Mamlaka ikiwemo kufuata Mpango wa Mafunzo.

Aidha, amewasisitiza kuhakikisha wanapata ruhusa ya maandishi kutoka kwa Wakuu wao, kabla ya kwenda masomoni kwani kinyume chake watakabiliwa na mashtaka ya utoro kazini ambayo adhabu yake ni kufukuzwa kazi.

 “Tumekuwa tukipata rufaa nyingi za kesi za Walimu ambao walitoroka kazini na kwenda masomoni hivyo kufukuzwa kazi. Serikali inapenda walimu msome lakini fuateni taratibu zilizowekwa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Mecktildis Kapinga, akifafanua kuhusu utaratibu wa kupanda vyeo, ameueleza Mkutano huo kuwa, kanuni inaelekeza kutompandisha cheo mtumishi yeyote wa umma akiwa masomoni, hadi pale anapohitimu ndipo mchakato wa kumpandisha hufanyiwa kazi.

“Naomba mtambue kuwa utaratibu huo ni kwa watumishi wote wa umma, na siyo kwa walimu pekee kama ambavyo baadhi yenu mmekuwa mkinung’unika,” amefafanua Kapinga.

Mkutano huo wa siku tatu, ulianza Januari 5, 2021 huku ukiongozwa na kaulimbiu isemayo uongozi na usimamizi makini wa elimu, utaimarisha Tanzania katika uchumi wa kati.

Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa walimu wa shule za msingi na sekondari Tanzania Bara, walio kwenye utumishi wa umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles