Susan Uhinga, Korogwe
Serikali imewataka wananchi kuwapokea na kuwapa ushirikiano walimu wa kujitolea kutoka katika Shirika la Huduma za kujitolea la Marekani la Peace Corps, ambao watakuwepo nchini kwa muda miaka miwili.
Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ameyasema hayo wakati wa shughuli ya kuwaapisha walimu 59 wa masomo Sayansi, Hisabati na Kiingereza kutoka nchini Marekani yalifanyika katika ukumbi wa chuo cha uwalimu wilayani Korogwe Mkoani Tanga.
Amesema walimu hao watakwenda katika wilaya 59 za mikoa tofauti nchini kwenye shule za sekondari.
“Wananchi mkawape ushirikiano walimu hawa ambao watakuwepo hapa nchini kwa miaka miwili wakitoa huduma ya kufundisha watoto wetu katika shule zetu za sekondari huduma hiyo wameapa hapa kwamba wataifanya bure kabisa,” amesema Ole Nasha.
Awali akisoma hotuba kwa mgeni rasmi, Mkufunzi wa lugha ya kiswahili ambaye alikuwa akiwafundisha walimu hao amesema wamekuwa na walimu hao kwa muda wa wiki tisa wakiwafundisha kuzungumza kiswahili pamoja na namna ya kuishi maisha halisi ya mtanzania.
“Tumeishi nao vizuri katika muda wa wiki tisa ambapo mbali na kuwafundisha lugha yetu lakini pia tumewafundisha maisha halisi ya Mtanzania kama vile kupika kwa kutumia kuni, kufua nguo kwa mikono na shughuli mbalimbali wameelewa na tunahakika watakwenda kuishi vizuri.” amesema mkufunzi huyo.
Kwa upande wao walimu hao wamesema kuelimisha jamii kunahitaji sera nzuri, serikali, pamoja na jamii iliyo tayari.
Walimu hao wanatarajia kuondoka kesho kuelekea katika vituo vyao vya kazi walivyopangiwa katika wilaya tofauti za mikoa ya Tanzania.