30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Walimu kizimbani kwa  kuiba mtihani wa taifa

NA KULWA MZEE-DAR EA SALAAM

WALIMU watano akiwamo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Kimataifa ya Hazina, wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashtaka ya kupata mtihani wa taifa ya darasa la saba na kuwaonyesha wanafunzi wa shule hiyo.

Shule ya Hazina ni shule inayong’ara katika matokeo ya darasa la nne na la saba na  mwaka huu imeongoza kwenye mtihani wa darasa la nne wakati mwaka jana ilikuwa miongoni mwa shule 10 bora kwenye matokeo ya darasa la saba.

Washtakiwa waliofikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka matatu yanayowakabili ni Mwalimu Mkuu, Patrick Cheche na wenzake, Mwalimu Laurence Ochien, Mwalimu Justus James, Mwalimu Nasri Mohammed na Mwalimu Mambo Iddi.

Washtakiwa walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na  Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono.

Washtakiwa wanadaiwa Septemba 5 mwaka huu walikula njama kuingilia mitihani ya taifa isivyo halali.

Katika shtaka la pili wanadaiwa Septemba 5, katika maeneo ya Shule ya Msingi Hazina Magomeni, kinyume cha sheria, walipata mitihani ya taifa na kwa makusudi waliwaonyesha watahiniwa wa shule hiyo.

Mwanaamini alidai shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote ambalo wanadaiwa tarehe iliyotajwa katika maeneo ya shule, kinyume cha sheria, walifanya mawasiliano na watahiniwa na kuwapa maudhui ya mitihani.

Washtakiwa walikana mashtaka.   Jamhuri haikupinga dhamana isipokuwa ilitaka sheria ifuatwe  kuwawezesha washtakiwa kufika mahakamani.

Kishenyi aliomba mshtakiwa Ochieng na James wawasilishe hati zao za kusafiria mahakamani sababu ni raia wa Kenya.

Hakimu Shaidi alitaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili, kati ya wadhamini hao mmoja atoke katika taasisi inayotambulika nakila mdhamini awe na barua na kitambulisho.

Vilevile, kila mdhamini atasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni sita. Mshtakiwa wa kwanza na wa pili waliamuliwa kuwasilisha hati zao za kusafiria.

Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana isipokuwa mshtakiwa wa pili ambaye anatakiwa kuwasilisha mahakamani hati yake ya kusafiria.

Kesi iliahirishwa  hadi Oktoba 10 mwaka huu itakapotajwa tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles