Na Clara Matimo, Mwanza
Wakuu wa Idara na Wataalamu kutoka sekta mbalimbali Mkoani Mwanza wametakiwa kwenda katika halmashauri zote nane zilizopo mkoani humo ili kushirikiana na wenzao wa maeneo hayo kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Agizo hilo limetolewa mkoani hapa Julai Mosi na Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel, wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi yake kwenye kikao kilicholenga kujadili masuala mbalimbali ya kiutumishi na maendeleo kwa mwaka wa fedha ulioishia juni 30, 2022.
Alieleza kwamba hivi karibuni amezunguka katika halmashauri zote za mkoa huo kwenye mkutano maalumu wa baraza la madiwani uliolenga kujadili utekelezaji wa hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2020/2021 amebaini changamoto kadhaa hivyo ni wajibu wa watumishi hao ngazi ya mkoa kuwasaidia ili kuziondoa na kuepuka matumizi mabaya ya fedha .
âHoja za CAG zipewe kipaumbele kwa mwaka mpya wa fedha ulioanza Julai Mosi, mwaka huu kwani mafanikio ya mtu mmoja ni Yetu sote na kushindwa kwa kitengo kimoja ni kushindwa kwetu wote tuangalie ndoto dira na mwelekeo wa serikali.
âTuweke malengo kwenye mwaka huu mpya wa fedha tunataka tufike wapi, malengo yanaokoa muda usipokuwa na malengo utabaki kuzunguka tu maana haujui unapokwenda, nawaombea kila mtumishi Mwenyezi Mungu awaongezee ufanisi wa ziada katika kutimiza majukumu yenu, vitengo vyote tuwe sehemu ya suluhu na ufanisi wa utendaji kazi,â alisema na kuongeza.
âMimi ninyi siwaoni kama ni wafanyakazi wenzangu nawaona kama ni ndugu zangu wa damu, kikao hiki mbali na kufanya tathmini kinatusaidia kujuana mkijuana mnaaminiana tujifunze kuombeana, kuvumiliana na kusameheana ili tufanye kazi zenye tija,âalisema.
Aidha amewataka kufanya tathmini ya kina ya vyanzo vya mapato ndani ya mkoa, ili kubaini vinavyohitaji maboresho maana mapato yakiongezeka wanajenga msingi mzuri katika kutatua changamoto mbalimbali ndani ya mkoa na taifa kwa jumla.
âTunapofungua mwaka mpya wa fedha 2022/23 tumekutana ili kufanya tathmini ya kazi tulizotekelezwa katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita hongereni kwa kazi nzuri mliyofanya mwaka huu mpya tuna deni kubwa katika kuwahudumia wananchi kupitia ofisi zetu hivyo pamoja na tathmini tunayoenda kufanya ni wajibu wetu kuongeza ushirikiano na kuombeana kheri katika kazi,âalisema.
Ametaja mafanikio ya kiutumishi kwa mwaka wa fedha  2021/2022 kuwa ni pamoja na watumishi 51 wa kada mbalimbali wamepandishwa vyeo kuanzia Juni 2021 hadi Mei 2022 na wengine idadi hiyo hiyo wamethibitishwa vyeo, kiasi cha Sh 436,749,786 kimelipwa kwa wazabuni waliokuwa na madai mbalimbali ya miaka ya nyuma.
âKiasi cha Sh 209, 167,830 kimelipwa kwa watumishi waliokuwa wakidai madai yasiyo ya mishahara, tumefanikisha kuandaa bajeti ya mishahara ya watumishi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo kiasi cha Sh 185,844,000 kimetengwa kwa ajili ya ajira mpya kati ya hizo 14 kada za udereva, RMAs, PSs pamoja na kupandishwa vyeo watumishi 29,âalisema Mhandisi Gabriel.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa huo  Ngusa Samike, amemshukuru  Rais Samia Suluhu Hassan,  kwa kuipatia Ofisi hiyo Sh Bilioni 1.75 ambazo zinatekeleza maboresho ya miundombinu pamoja na ujenzi wa nyumba za Makatibu Tawala Wasaidizi, Ukarabati wa Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Ujenzi wa Ofisi za Maafisa Tarafa.