29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi waliounguliwa na bweni Bwiru Sekondari wafutwa machozi

Na Clara Matimo, Mwanza

Baada ya bweni la wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru iliyopo wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, kuungua moto usiku wa Juni 29, mwaka huu saa 3:45 wadau mbalimbali wametoa misaada kwa wanafunzi walioaunguliwa na vifaa vyao ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao.

Wadau ambao wamewafuta machozi wanafunzi hao ni pamoja na Taasisi ya Desk and Chair Foundation, inayojishughulisha kutoa misaada mbalimbali kwa jamii katika maeneo yenye uhitaji, imetoa magodoro, vyandarua na shuka mbili kwa wanafunzi wote 76 ambao vifaa vyao viliteketea kwa moto vyenye thamani ya Sh milioni 3,458,000,  benki ya NMB imechangia mabati bando 11 zilizogharimu Sh milioni tano ili kuwezesha kukamilika kwa ujenzi wa bweni jipya.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, wadau wengine walioguswa na kuchangia mahitaji mbalimbali ya wanafunzi hao ikiwemo viatu, sweta, vyombo vya kulia chakula, suruali, mashati ya shule, masanduku ya chuma ya kuhifazia vifaa vya shule(trunker) na kufuli ni kiwanda cha Nyakato Steel Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dk. Angeline Mabula na wengine ambao hawakutaka kutajwa majina yao.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa wanafunzi, Juni 30, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Gabriel, aliwashukuru wadau hao kwa moyo wa ukarimu waliouonyesha kwa wanafunzi hao huku akiwataka wazazi, walezi na wananchi  kutokuwa na hofu  kwani watoto wote shuleni hapo  wapo salama na wanaendelea na masomo yao kama kawaida  vilevile kamati ya maafa ya mkoa itahakikisha wanapata mahitaji yote ambayo yaliteketea kwa moto.

“Nawaagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilayya ya Ilemela hakikisheni ujenzi wa bweni jipya unakamilika mapema iwezekanavyo  wadau wametusaidia vifaa mbalimbali vya ujenzi ili watoto wetu wasipate shida eneo la kulala, vifaa wamepata na watapata vyote maana wadau ni wengi ambao wameishaahidi kusaidi, vifaa vyote wanavyopewa  ni vyao haya magodoro mtumishi yeyote asiwanyang’anye ni yao maana walipokuja walikuja na godoro zao,”alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Desk and Chair Foundation,Tawi la Tanzania, Alhaji Sibtain Meghjee, aliwaasa wanafunzi hao kutopata hofu wala kuvunjika moyo katika masomon yao  kutokana na   changamoto iliyowakuta bali wazingatie  masomo  na waendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ili awaepushe na majanga.

“Nyie vijana ndiyo viongozi wa kesho mnaweze mkawa kwenye nafasi ya juu ya uongozi kama alivyo mkuu wa mkoa wetu leo Mhandisi Gabriel, hata sisi tumepitia changamoto mbalimbali katika safari yetu ya masomo kikubwa endeleeni kumuomba Mwenyezi Mungu ili awaepushe na majanga na mzingatie masomo yenu maana kupata nafasi kwenye shule hii ni kazi kubwa sana nyie mnabahati ya pekee kuwa katika shule hii ya Bwiru Boys enzi zetu tulitamani kuja hapa tukafeli,”alisema Alhaji Meghjee.

Naye Meneja wa Kanda ya Ziwa Benki ya NMB, Ladislaus Baraka, alisema wametoa  mabati 132 vyenye  thamani ya Sh milioni tano ili yasaidie  kuezeka jengo ambao limeandaliwa kwa ajili ya watoto ambao bweni lao liliungua ikiwa ni kutekeleza sera  yao ya kurudisha fadhira kwa jamii.

“Benki ya NMB inao utaratibu wa kushiriki  na kushirikiana na serikali pamoja na jamii inayotuzunguka kama sehemu ya uwajibikaji wetu kwa jamii kurejesha sehemu ya faida tunayoipata kwa ajili ya kusaidia eneo la majanga, ndiyo maana tumeamua kuja kuungana na wenzetu wa shule hii kutoa vifaa vya kuezekea, NMB tunasema tuko karibu yako na wewe zaidi ndiyo maana leo tuko hapa,”alisema Baraka.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mulunga Bahebe, aliiambaia Mtanzania Digital kwamba wametoa kiasi cha Sh milioni 42 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni hilo ambapo tayari lilikwisha fikia hatua ya lenta.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Salum Kalli, alisema “Tunakushukuru sana Mhe Mkuu wa Mkoa Mhandisi Gabriel,  kwani usiku wa jana (juzi) ulituahidi kuwa ndani ya saa 24 vifaa vilivyoteketea vitapatikana na kwa maelekezo uliyoyatoa tunakuahidi tutatumia siku tatu tu tunakamilisha ujenzi wa jengo la bweni lililo pale juu, “alisema.

Nao baadhi ya wanafunzi ambao ni wahanga wa tukio hilo akiwemo Shadrack Joseph, Peter Joseph na Andrew Yesaya, waliishukuru serikali inayoongwa na Rais Samia Suluhu Hassan  kwa kuwaleta kiongozi mwenye upendo Mhandisi Gabriel ndani ya mkoa huo ambaye amekuwa nao tangu usiku tukio lilipotokea na amewatafutia  wadau hao walio wawezesha   vifaa vyote vilivyoteketea  huku wakiahidi kwamba watasoma kwa bidii ili waje walitumikie taifa hapo baadaye.

Awali, Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Thomas Werema, alisema moto umeteketeza vifaa vyote vilivyokuwemo kwenye bweni la wanafunzi majira ya saa 3 usiku wakati wanafunzi wakiwa darasani wanajisomea na waliopata majanga ni wanafunzi 76 lakini wote wapo salama hakuna aliyedhurika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles