28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Wakulima, wavuvi watakiwa kulipa kodi

Na Nyemo Malecela, Kagera


WAKULIMA, wafugaji na wavuvi wametakiwa kulipa kodi asilimia mbili kila watakapouza bidhaa zao moja kwa moja katika kampuni zinazoongeza thamani ya bidhaa hizo.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Msimamizi wa kodi Mkoa wa Kagera (TRA), Alex Mwambenja katika semina ya kuwashirikisha wafanyabiashara na walipa kodi kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni, mwaka huu na kuanza kufanya kazi Julai Mosi, 2021.


Amesema endapo wakulima, wafugaji na wavuvi watauza mazao yao kwenye vyama vya ushirika hawatalipa kodi hiyo na badala italipwa na vyama vya ushirika vikiuza bidhaa hizo kwenye kampuni.


“Hivyo kama kuna wakulima, wafugaji na wavuvi watataka kuuza bidhaa hizo moja kwa moja kwa kampuni wanatakiwa kuwa na TIN na vitambulisho kwa kuwa kampuni hizo lazima ziwakate kodi hivyo itakuwa vema watambulike,” amesema.


Alex amesema serikali imeweza kuondoa kodi ya ongezeko la thamani katika vifaa mbalimbali vikiwamo vifaa vya kubebea maziwa wakati kwenye bima ya ufugaji imeweka msamaha kwenye VAT.
“Lengo la serikali kuondoa kodi hizo ni kuchochea ufugaji na unywaji wa maziwa yanayozalishwa nchini,” amesema.


Pia Alex ametolea ufafanuzi wa kodi ya majengo kwa nyumba zenye umeme ambayo itakusanywa na shirika la Umeme Tanesco kupitia luku, kila mteja atakapoingiza umeme.
“Tanesco wamepewa mamlaka zote za kukusanya kodi hiyo na kwa maelekezo yaliyotolewa na serikali ni kwamba kila nyumba inatakiwa kulipia shilingi elfu moja ya kodi ya majengo kwa mwezi.
Hivyo nyumba yenye mita za umeme zaidi ya moja, kiwango hicho cha fedha kitagawiwa kwa idadi ya mita zilizomo ndani ya hiyo nyumba.


“Na wafanyabiashara wa vitenge wametakiwa kutumia njia halali za forodha kuingiza bidhaa hizo nchini ili kuepuka kutaifishwa au kupata usumbufu mwingine endapo wataziingiza kupitia njia za magendo,”amesema.


Amesema tayari serikali imepunguza kodi ya bidhaa hiyo kwani kitenge chenye ukubwa wa mita moja kitalipiwa kodi ya 0.7 mpaka dola moja za Marekani na 0.8 mpaka dola moja za kimarekani kwa kitenge kilichotengenezwa kwa kutumia pamba.
Pamoja na mabadiriko ya sheria za kodi mbalimbali, TRA Mkoa wa Kagera wanatakiwa kukusanya kodi shilingi bilioni 83 kwa mwaka huu wa fedha.


Kwa mwaka 2020/2021 TRA Mkoa wa Kagera imeweza kupata walipa kodi wapya 3000 na zoezi hilo bado linaendelea ili kuweza kutimiza malengo ya kukusanya kiwango cha kodi kwa Mkoa.
Kwa upande wake mfanyabiashara Justice Kandokora, amesema wamiliki wa majengo wamekuwa wakipata usumbufu wa kodi za majengo wanapoenda kulipia kodi hiyo TRA, jambo linalosabishwa na mamlaka hiyo kuwatumia watendaji wa mitaa.

Amesema watendaji hao wamekuwa wakiandika majina tofauti na wamiliki wa nyumba, jambo ambalo usababisha mmiliki wa nyumba anapokwenda kulipia kodi anajikuta nyumba yake imeandikwa majina mawili na kulazimishwa kwenda mahakamani kuapa ili kulikana jina moja ambalo sio lake.

“Ushauri wangu maafisa wa TRA wanatakiwa wafanye uhakiki wa majengo hayo pasipo kuwahusisha watendaji wa mitaa ambao wameonekana hawako makini na kazi hiyo,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles