Na Derick Milton, Meatu
Mkuu wa mkoa wa Simiyu David Kafulila, amesema kuwa ndani ya siku tano kuanzia leo, wakulima wote wa zao la pamba Mkoani humo ambao bado hawajaondoa masalia kwenye mashamba yao, kuhakikisha wanaondoa mara moja kabla ya siku ya ijumaa ya wiki hii.
Kafulila amesema kuwa kuondoa masalia kwenye shamba kwa mkulima wa zao la pamba ni sheria wala siyo hiari, ambapo ameleza hadi kufikia siku hiyo kila mkulima wa zao hilo anatakiwa kuwa ameteleleza agizo hilo la kisheria.
Kiongozi huo ametoa agizo hilo leo Oktoba 11, 2021 wakati akiongea na viongozi, wakiwemo watendaji wa kata katika Wilaya ya Meatu Mkoani humo kwenye kikao cha kujadili jinsi mkoa huo utakavyoweza kuzalisha tani laki tano katika msimu mpya wa zao hilo.
Amesema kuwa sheria inaelekeza kila mkulima kuondoa masalia pamoja na magugu kwenye shamba lake, na ambaye atakaidi atatakiwa kutozwa faini kiasi cha Sh 50,000 au kifungo jela miezi sita au vyote kwa pamoja.
Amewataka watendaji wa kata kuhakikisha baada ya muda huo uliotolewa kuisha, wanatekeleza kwa vitendo sheria hiyo kwa mtu yeyote ambaye atakaidi kutii, kwani mkoa huo umejidhatiti kuhakikisha unazalisha kiasi hicho cha pamba katika msimu huu.
“Kufika siku ya ijumaa wiki hii hakuna shamba lolote kubaki na masalia, wala magugu, wakulima wote wanatakiwa kusafisha mashamba yao, watendaji wa kata mnatakiwa kusimamia hilo, kama kuna shamba litabaki Mtendaji wa kata, Kijiji lazima ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua kali” amesema Kafulila….
“Kwa wale ambao watakaidi, wakamatwe mara moja na kufikishwa mahakamani, lazima sheria itekelezwe hakuna mtu aliyeko juu ya sheria, Mtendaji atakayeshindwa ni kwamba atakuwa ameshindwa kutimiza majukumu yake, na atatakiwa ajieleza kwa nini asichukuliwe hatua kali,” ameongeza Kafulila.
Katika kikao hicho Mkuu huyo wa mkoa amewataka watendaji wote ndani ya Wilaya hiyo pamoja na maafisa kilimo na ugani, kuhakikisha wanawasaidia wakulima ili waweze kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba na mkoa kuweza kufikia malengo yake.
Amesema kuwa katika mpango mkakati, mkoa wa Simiyu imejiwekea lengo la kuzalisha tani laki tano msimu wa 2021/2022 hali ambayo itafanya nchi kuwa kinara wa uzalishaji wa zao hilo katika baraa Afrika.
“Lazima wakulima wawezeshwe kila kitu, Elimu na pembe jeo kwa wakati na kwa urahisi, kila mkulima lazima apande kwa vipimo, aweke mbolea, kunyunyuzia viuatilifu na kupata mbegu kwa wakati, tutahakikisha mahitaji yote yanapatikana kwa wakulima,”alisema Kafulila.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Fauzia Hamidu amesema kuwa Ofisi yake imeanza mkakati wa kuhakikisha inatembelea kila kijiji kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima jinsi ya kuhakikisha wanalima kwa kufuata kanuni bora za kilimo hicho.