22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau haki za mtoto wa kike washauri wafanyakazi wa nyumbani kupata mikataba

Na Clara Matimo, Mwanza

Katika kuhakikisha haki za mtoto wa kike zinazingatiwa na kulindwa, wadau wa masuala ya wanawake na watoto jijini Mwanza wameshauri kuwe na ulazima katika ajira za wafanyakazi wa nyumbani wapatiwe mikataba na mazingira rafiki ya kazi.

Pia wameiomba serikali kuwachukulia hatua wazazi na walezi wote watakaobainika kuwatumikisha watoto chini ya umri wa miaka 14 kwa kuwapeleka kwenye ajira hali inayosababisha washindwe kutimiza ndoto zao kupitia elimu na wale wanaotumia watoto kama chanzo cha mapato yao.

WASHIRIKI : Baadhi ya washiriki wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyoandaliwa na mashirika yasiyo ya serikali ya WoteSawa linalojishughulisha kutetea haki za mfanyakazi wa nyumbani na Railway Children Africa, linalotetea haki za watoto na vijana wanaoishi na kufanya kazi mtaani wakisikiliza shuhuda zinazotolewa na washiriki wenzao Picha na Clara Matimo.

Wadau hao kutoka mashirika yasiyo ya serikali ya WoteSawa linalojishughulisha kutetea haki za mfanyakazi wa nyumbani na Railway Children Africa,linalotetea haki za watoto na vijana wanaoishi na kufanya kazi mtaani wametoa wito huo leo jijini hapa katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike kimataifa  inayoadhimishwa Oktoba 11, kila mwaka yaliyobeba kauli mbiu ‘kizazi cha kidigital kizazi chetu’.

Wamesema endapo kutakuwa na ulazima wa kila mwajiri kumpa mkataba mfanyakazi wake wa nyumbani itasaidia kuihamasisha jamii kutambua umuhimu wa kulinda maslahi ya wafanyakazi wa nyumbani ambao baadhi yao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili na malipo duni kutoka kwa waajiri wao.

Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Wotesawa, Masesa Bandoma, amesema baadhi ya wazazi na walezi wanawaruhusu watoto wao walio na umri wa miaka 14 kuendelea kufanya kazi mbali mbali hasa za nyumbani lakini mshahara wanachukua wao na mtoto ambaye ndiye anayewajibika hanufaiki na kazi anayoifanya huo ni ukatili wa kijinsia.

“Naiomba serikali kupitia siku ya leo ya mtoto wa kike iwashughulikie kikamilifu wazazi na walezi wa aina hii ambao watabainika kuchukua mishahara ya watoto wao kwa sababu mtu anapofanya kazi anastahili alipwe mshahara ambao utakuwa na manufaa kwake pamoja na waajiri watakaobainika kuwalipa wafanyakazi wao wa nyumbani wanaoishi nao mshahara chini ya elfu 40 nao wachukuliwe hatua maana wanavunja sheria, hizi ni miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo watoto wa kike,” amebainisha Bandoma.

Mwanasheria wa Shirika la Railway Children Africa, Anitha Joseph, ametaja changamoto wanazokutana nazo katika utendaji wao wa kazi kuwa ni pamoja na  jamii kuwa na mtazamo hasi kwa watoto hao ambao wanaishi na kufanya kazi mtaani.

“Tunapofanya kazi ya kuwasaidia watoto hawa jamii  inatuona kama tunafanya kazi na majambazi, baadhi wanasema shirika letu linawatumia watoto hao ili kujipatia  mtaji pia baadhi ya familia za watoto hao zinatuchukulia kama ni freemason kwa sababu tunapowaokoa watoto kutoka mtaani walio na umri chini ya miaka 14 huwa tunawarudisha nyumbani kwao na tunaendelea kuwafuatilia sasa tunapowafuatilia ili kujua kama wanaendelea na masomo  ndiyo tunapokutana na hayo walio na umri zaidi ya miaka 14 tunawasaidia kutimiza ndoto zao kwa kuwapa mitaji na kuwapangia nyumba za kuishi.

“Naiomba jamii ijihusishe kwa asilimia mia moja kwenye malezi ya watoto, ikifanya hivyo hatutakuwa na watoto wa mitaani maana tangu tumeanza shughuli ya kuwasaidia watoto hao hatujawahi kukutana na mtoto ambaye hana familia, hata kama wazazi wake wote wawili wamefariki lakini lazima anao ndugu wa baba au mama yake, watoto wanapoingia mtaani hasa wa kike wanakutana na changamoto nyingi tuwalinde,” amesema Anitha.

Naye Mkaguzi wa polisi kutoka dawati la jinsia Igogo, Gloria Shindika, amewataka watoto wa kike kuripoti matukio mbalimbali ya ukatili wanayofanyiwa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria vilevile kesi zinapofika mahakamani wasitishwe waende wakatoe ushahidi.

“Jeshi la polisi linaendelea kutoa elimu ya uelewa kwa jamii kuhusiana na haki zao hasa kwa kundi la wanawake ambao wengi wao wanakutana na ukatili wa kingono wanabakwa, wanaingiliwa kinyume na maumbile, ukatili wa kimwili kama kupigwa, ukatili wa kisaikolojia kama kutukanwa yote hayo ni makoza ya jinai, nawaomba watoto wa kike mkifanyiwa vitendo hivyo msikae kimya toeni taarifa sio tu kituo cha polisi nenda karipoti hata kwenye ofisi ya serikali ya mtaa ili tukomeshe vitendo hivi,”amesisitiza.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Afisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza, Betty Mtega, amesema  serikali inaendelea kufanya ukaguzni mahali pa kazi lengo ni kuhakikisha sheria za nchi zinalindwa na miongozo mbalimbali inafuatwa ili kuendeleza juhudi za usawa wa kijinsia.

Maadhimisho hayo yamewakutanisha baadhi ya wafanyakazi wa nyumbani kutoka maeneo mbalimbali jijini humo, watoto  na vijana waliookolewa na mashirika hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka jiji la Mwanza, Idd Maketa, wanufaika wa mashirika hayo ambao wamewezeshwa kwa kupewa mafunzo ya fani tofautitofauti na mitaji, waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani na wadau mbalimbali wanaotetea haki za mtoto wa kike.

MWANASHERIA:  Mwanasheria wa Shirika la Railway Children Africa, Anitha Joseph, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike kimataifa jijini Mwanza leo, iliyoratibiwa na shirila hilo pamoja na Wotesawa. Picha na Clara Matimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles