24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

Bonaza la Caflo lafanikisha elimu mapambano dhidi ya VVU

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mashindano ya mpira wa pete na michezo mingine yamesaidia kufikisha elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU kwa vijana wa Kata za Buguruni, Vingunguti, Mnyamani, Tabata na Kipawa.

Mashindano hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Sinai Vingunguti yameandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la CAFLO ambalo linatekeleza mradi wa kudhibiti maambukizi ya VVU katika kata hizo.

Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Barnabas Kisai, akikabidhi mbuzi kwa timu ya Majumba Sita iliyoibuka mshindi katika mashindano ya mpira wa pete wakati wa bonaza la Caflo lililokuwa na lengo la kuhamasisha vijana kujikinga na maambukizi ya VVU. Wapili Kushoto ni Mwenyekiti wa CAFLO, Mariam Mlugu.

Katika mashindano hayo timu ya Peace and love kutoka Mnyamani iliibuka mshindi katika mchezo wa mstari kati na kuzawadiwa mbuzi mmoja wakati Majumba Sita Queens kutoka Kipawa walinyakua ushindi wa mpira wa pete na kuzawadiwa mbuzi.

Aidha katika mashindano ya mpira wa miguu Mnyamani Youth Initiative kutoka Kata ya Mnyamani iliibuka mshindi na kuzawadiwa mbuzi.

Pia kulikuwa na mashindano ya kukimbia kwa viroba, kuvuta kamba, kukimbiza kuku na kuimba.

Mwenyekiti wa CAFLO, Mariam Mlugu, amewataka vijana hao wakawe mabalozi kwa kuwafundisha wenzao elimu ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Amesema mradi huo umewalenga vijana wenye umri wa kuanzia miaka 14 hadi 25 waliopo katika kata hizo kwa sababu ndiyo kundi linaloonekana kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU ikilinganishwa na makundi mengine.

Alisema pia wamefanikiwa kuunda na kuendeleza majukwaa ya vijana hususani wasichana kwa lengo la kuwawesesha kupata elimu na mbinu ya kujikinga na VVU na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za kukuza uchumi na kuleta maendeleo.

“Tunaamini kwamba vijana wakipata fursa ya kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi ni njia mojawapo ya kuwawezesha kujikinga na maambukizi ya VVU,” amesema Mlugu.

Mwenyekiti huyo amesema kupitia mradi huo pia waliendesha midahalo kwa wanafunzi wa shule za sekondari ili kuwaelimisha kujikinga na maambukizi ya VVU.

Mgeni rasmi katika mashindano hayo Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Barnabas Kisai, amelipongeza shirika hilo kwa kufikisha elimu ya Ukimwi kwenye jamii kupitia mashindano hayo.

“Kutokana na hamasa kubwa tuliyoiona katika bonaza hili tunafikiria maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanayoadhimishwa Desemba Mosi tuyalete Vingunguti,” amesema Kisai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles