Na Ashura Kazinja, Morogoro
BODI ya Pamba Tanzania imewataka wakulima Kanda ya Mashariki kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili kuondokana na umaskini kutokana na kupanda kwa bei hadi kufikia Sh 1,560 kwa kilo pamoja na kuwepo kwa soko la uhakika.
Meneja wa Huduma za Usimamizi wa Bodi ya Pamba Kanda ya Mashariki, Emmanuel Mangulumba amesema hayo kwenye maonesho ya wakulima kanda ya mashariki yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Mororgoro, ambapo ameeleza kuwa kilimo cha pamba hulimwa katika kanda mbili ambazo ni kanda ya magharibi yenye mikoa 12 na kanda ya mashariki yenye mikoa mitano ambayo ina mikoa ya Iringa, Tanga, Morogoro, Kilimanjaro na Pwani.
Amesema mpaka sasa uzalishaji kitaifa ni kwamba asilimia 99 huzalishwa kanda ya magharibi na mashariki huzalisha asilimia moja hadi chini ya asilimia moja lakini azimio la Serikali ni kuwatoa kwenye umasikini wananchi kupitia kilimo cha pamba, ambapo zao la pamba lilianzia kanda ya Mashariki maisha ya watu yalikuwa mazuri sana na kwamba kupitia zao hilo serikali imeona kuwa wananchi wanaweza kutoka kwenye umaskini.
“Msimu uliopita wa mwaka 2021 kiwango cha uzalishaji kilikuwa kilo 314,000 na kwa msimu huu wa 2022 tunategemea kuzalisha mara 10 zaidi ya kiwango hicho kutokana na jitihada zinazofanyika kupitia wadau mbalimbali ikiwemo bodi ya pamba wenyewe na Mwekezaji ‘Upami Agrobissiness’ ambao wanahamasisha kilimo cha pamba kwa wakulima katika eneo lote la kanda ya Mashariki.
“Tunaendelea na jitihada za kuwasaidia wakulima wa pamba kwa mbegu, mbolea na pembejeo kwa mkopo ili kilimo hicho kiweze kuboreshwa kwenye kanda ya mashariki,” amesema.
Nae Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwekezaji wa Pamba, Upami AgroBusiness Ltd, Vitus Lipagila amesema anajipanga kuhakikisha pamba inalimwa zaidi kanda ya mashariki kwa sasa na kuondoa changamoto ya wakulima kukosa soko baada ya kuwepo wanunuzi wanaotoka kanda ya magharibi pekee.
Lipagila amesema tayari kampuni yake imeshafufua viwanda viwili vya kuchakata Pamba ambavyo vipo katika wilaya za Kiku – Kilosa na Koreko cha mkoa wa Pwani ambavyo tayari ameshaingia navyo mkataba na vinafanya kazi kwa sasa na kuondoa ugumu uliokuwa kwa wakulima na wanunuzi ambao walitoka mbali kwenye mikoa kama ya Singida na kwamba anatarajia kujenga kiwanda kikubwa Lupilo- Mahenge wilayani Kilombero mkoani hapa.
Alisema kwa msimu wa kilimo wa mwaka huu kanda ya Mashariki wanatarajia kuvuna kilo milioni 2 na ambazo ni mwanzo mzuri sababu ni kitu ambacho hawakutegemea kabisa.
Aidha, aliwataka wakulima kuondoa hofu ya kuuza kwa mkopo bali kwa sasa wao Upami wananunua kwa pesa taslimu na kufanya wakulima kuendelea kunufaika na zao hilo katika kutatua changamoto zao za kifamilia kwenye maisha yao ya kila siku.
Naye Afisa Kilimo zao la pamba kanda ya Mashariki, Alphonce Ngawagala aliwataka wakulima kuzingatia vipimo vya upandaji pamba katika mashamba yao ili kupata uzalishaji wa kutosha.
Ngawagala amesema kabla hawajaanza hamasa tayari wakulima wameshaanza kuongeza kulima zao hilo ambapo kwa msimu watakaoenda wa kilimo wa mwaka 2023 tayari wakulima wameshaonesha nia ya kuongeza kilimo na wanahitaji pembejeo mbegu.
Alisema msimu huu wa kilimo pamba ipo shambani inavunwa na wengine wameshaanza kuuza, na kwamba wakulima kwa sasa wana jumla ya hekari 9,579 tofauti na awali ambapo walikuwa na ekari 3,000.