GRACE SHITUNDU Na DERICK MILTON – SIMIYU
WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, amezindua bima ya mazao iliyo chini ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) na kulitaka kuhakikisha linayafikia mazao yasiyopungua matano ndani ya mwaka mmoja.
Bima ya mazao ambayo imezinduliwa kwa mara ya kwanza katika maonyesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi, Simiyu itaanza kufanya kazi katika zao la pamba mkoani humo na baadaye wataenda kwa wakulima wa kahawa mkoani Kagera.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Hasunga alisema uzinduzi wa bima ya mazao ni mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo kwani itawasaidia wakati wa majanga mbalimbali.
“Nilipoteuliwa katika wizara hii nilijiwekea malengo ambayo miongoni mwa malengo hayo ni kuwa na bima ya kilimo, nimefurahi kwamba Shirika la Bima la Taifa limekuwa la kwanza kutekeleza.
“Mmeanza na zao la pamba katika Mkoa wa Simiyu na mtaenda kwenye kahawa Kagera. Ni jambo nzuri, lakini nataka ifikapo mwakani mmeshayafikia mazao yasiyopungua matano ili wakulima waweze kuwa na uhakika wa uwekezaji katika kilimo,” alisema Hasunga.
Alisema kwamba wakulima watanufaika na aina tatu ya bima katika bima hiyo ya mazao.
“Bima ya kwanza ni Bima Mseto ambayo inahusika na mazao yatayoathiriwa na ukame, upepo mkali, wadudu, moto, radi, barafu, mafuriko na tetemeko.
“Bima ya pili ni Hali ya Hewa na ya tatu ni Bima ya Maeneo maalumu ambayo inahusika na upungufu wa mazao, yaani mkulima alitarajia kupata magunia kadhaa, lakini kutokana na hali ya hewa akavuna pungufu, bima hii itamuhusu,” alisema.
Alisema baada ya kufanikisha suala la bima, pia wizara yake itashughulika na sera ya kilimo, sheria ya kilimo na takwimu za kuonyesha kuna wakulima wangapi na wanalima nini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dk. Elirehema Doriye, alisema bima hiyo itawasaidia wakulima katika majanga kama magonjwa, ukame, wanyama vamizi wa mazao na mafuriko.
Elirehema alisema kuwa faida itamkomboa kulima katika kilimo kidogo kwenda kilimo cha kisasa bila ya kuwa na hofu ya kupoteza mtaji alioweka shambani.
Alisema bima hiyo pia itamsadia mkulima kupata mkopo katika benki za kibiashara na kilimo.
“Ni vyema wakulima wakajiunga na bima hiyo na kuliamini shirika la NIC kwa kuwa ni mali ya Serikali, hivyo ni mali yao pia,” alisema.
Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika, Dk. Titus Kamani, aliwashauri wakulima kujiunga katika vyama vya ushirika ili kurahisisha upatikanaji wa bima ya mazao kwa wakulima.
“Kilimo kilikuwa kinapata changamoto nyingi, sasa kuzinduliwa kwa bima hii ya mazao kutawasaidia wakulima na ninawashauri wakulima kujiunga katika ushirika ili kufanikiwa na kuwa na uhakika wa mazao yao,” alisema Dk. Kamani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema kuwa wao kama mkoa wako tayari kutekeleza bima hiyo.
Alisema sekta ya kilimo katika kipindi hiki haihitaji maneno mengi, bali vitendo na utekelezaji.
“Katika sekta hii kumekuwa na matamko mengi, kama kilimo ni nguvu, kilimo kwanza, lakini hakuna matokeo yanayoonekana, sasa tunataka tukija hapa mwakani tuje na matokeo chanya yanayoonekana kwa vitendo.
“Wawepo kweli wakulima ambao watakuwa wamejiunga na bima hiyo na kujiwekea uhakika wa mazao yao,” alisema Mtaka.