31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wakili wa Zitto adaiwa si raia

Na Waandishi Wetu, DAR, MOSHI

Albert Msando
Wakili wa Zitto Kabwe, Albert Msando

anayemtetea Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amehojiwa na Idara ya Uhamiaji mkoani Kilimanjaro akitakiwa kueleza uhalali wa uraia wake wa Tanzania.

Msando  anamtetea Zitto katika kesi yake   dhidi ya uongozi wa Chadema katika  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam akipinga uanachama wake kujadiliwa na Kamati Kuu ya chama hicho.

Kutokana na kesi hiyo Mahakama Kuu   ilizuia chombo chochote cha Chadema kutojadili suala la uanachama wa Zitto hadi Baraza Kuu la chama hicho litakapojadili rufaa yake.

Msando mwenyewe aliiambia MTANZANIA Jumamosi kuwa aliitwa Uhamiaji mwezi mmoja uliopita na kutakiwa kutoa vielelezo   kuthibitisha uraia wake.

Idara ya Uhamiaji pia imemtaka apeleke cheti cha kuzaliwa, cheti cha ubatizo na barua ya utambulisho kwenye ofisi za idara hiyo  keshokutwa.

MTANZANIA Jumamosi ilimtafuta Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro,Johaness Msumule, ambaye alikiri kuhojiwa kwa Msando ingawa alikataa  kulizungumzia suala hilo kwa undani akidai lipo katika uchunguzi wa awali.

“Siwezi kuzizungumzia taarifa hizo   kwa sasa kwa sababu bado ni mbichi… nitafute wakati mwingine,” alisema Msumule.

Hata hivyo, Msando, alisema  pamoja na kutoa maelezo hayo alipewa fomu maalumu aeleze uraia wake.

Msando alisema pia kuwa baba yake mzazi, Gasper Msando na kaka yake mmoja walihojiwa juzi na maofisa wa idara hiyo.

“Ndugu zangu waliulizwa kuhusiana na suala langu. Kwa kweli mambo haya yamenishangaza sana,” alisema Msando  ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mabogini mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya Chadema.

Msando alisema   mama yake mzazi, Theresia Msando na dada yake, Acquilina Gasper, nao wametakiwa kufika ofisi za   Uhamiaji mkoani Kilimanjaro, keshokutwa.

Wakili huyo alisema ameshangazwa na tuhuma hizo kwa sababu yeye ana asili ya Mkoa wa Kilimanjaro ambako wazazi wake walizaliwa.

Alisema alizaliwa Novemba 8, 1979 na kusoma Shule ya Msingi ya Chekereni na Shule ya Sekondari ya Uru, zote za mkoani humo.

“Nilimaliza kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Ilboru mwaka 1997 kabla ya kusomea Shahada ya Kwanza ya Sheria,” alisema Msando.

Msando alisema   baba yake alikuwa mfanyakazi wa lililokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) hadi lilipovunjwa na pia mama yake kwa nyakati tofauti amekuwa mratibu wa elimu na mwalimu wa kawaida.

Juzi, Msando, aliandika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook  kuwa; “Leo (juzi) Julai 26,2014 nilipeleka maelezo yangu ofisi ya Uhamiaji Moshi kuhusu uraia wangu. Kwa maelezo niliyopewa awali kuna wanaosema mimi siyo Mtanzania.

“Kutokana na hilo Mzee wangu, Gaspar Mwaria Msando na kaka yangu, George Mwaria Msando wamehojiwa juzi kama wananifahamu.

“Miaka 34 baada ya kuzaliwa hospitali ya serikali, kusomeshwa shule ya msingi ya serikali, shule ya sekondari ya serikali na chuo kikuu cha Serikali leo natakiwa kuelezea kama ni raia.

“Najiuliza, kama siyo raia mbona narudisha gharama zote za serikali? Je, nitaenda wapi kama leo hii mimi si raia? Stateless person(mtu ambaye si raia wa taifa lolote)?” ilisema taarifa hiyo ya Msando.

Hata hivyo,   Zitto, aliponda hatua hiyo akisema ni kichekesho cha aina yake.

Katika mtandao wake wa Facebook, Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC)alisema huenda kuna mtu anatafutwa katika suala hilo.

“Eti Albert Msando siyo raia wa Tanzania! Hii nchi ni vichekesho. Albert… wanajua wanayemtafuta? Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi aliwaambia wanachama Jukwaa la Wahariri (TEF)kuwa mimi Zitto Kabwe ni Mkongo.

“Albert, watakusumbua sana. Tutawashinda tu. Hatushindwi vita,” alisema Zitto.

MTANZANIA lilipomtafuta Zitto  kupata undani wa kauli yake, mbunge huyo alisisitiza kwamba kitendo hicho ni cha kinyama na kisichostahili.

“Ni unyanyasaji dhidi ya ubinadamu, hata hivyo tutashinda,” alisisitiza Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Haya ya furani ni kabira furani tumeyazoea haya tija waja hasali kijamii na kitaifa ni malumbano ya kisiasa na wanasiasa kwa masilahi yao. Mkapa alisema Kaborou ni Mzambia,akamjibu na yeye ni mmakonde wa Musumbiji yakaisha. Tukaambiwa Ulimwengu ni mnyarwanda yakaisha; Mungai mkikuyu, Zitto mkongo, inawezekana hizi ni asili zao na sio uraia wao, uraia wao ni Watanzania waliopewa na katiba ya nchi; kabira sio uraia , Mtanzania kama ni mwaarabu na muhindi toka wapi huko sijui, tunashangaa majirani wa damu ya kongo, musumbiji, kenya n.k. kuwa watanzania ?????? Kila mtu ana asili yake Obama asili yake Kenya uraia Mmarekani.Serikali/uhamiaji msijiingize kwenye mambo ya ngoswe/wanasiasa waachie wenyewe msitupotoshe wananchi, mbunge na diwani ni raia asili yao ni historia tu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles