25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

Muswada wa sheria ya kodi waota mbawa

Anne Makinda
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda

NA ESTHER MBUSSI, DODOMA

MISWADA ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Utawala wa Kodi, imeota mbawa na kusababisha mpasuko bungeni.

Uamuzi huo ulitangazwa jana na Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye alisema muswada huo hautajadiliwa katika mkutano huu ili kutoa fursa kwa kamati nyingine za Bunge zaidi ya Kamati ya Bajeti kushughulikia muswada hiyo.

Spika Makinda akitangaza uamuzi huo, aligeuka mbogo kwa wabunge na waandishi wa habari akiwatuhumu kuifanyia majungu Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti kwamba imenunuliwa na wafanyabiashara.

Kamati hiyo imekuwa ikilalamikiwa kuhongwa na wafanyabiashara ili wasitoe misamaha ya kodi kama unavyoelekeza muswada huo.

Alisema miswada hiyo inagusa sekta mbalimbali na pia ni miswada mizito ambapo kamati ya Bajeti ilijikuta haikuwaita wadau.

“Sasa usipowaita wadau ukatunga mwenyewe kesho ikishindikana inakuwa ni tatizo la Bunge, kwa hiyo tutaahirisha hadi Bunge linalofuata ili kamati husika zifanye kazi nzuri na baadaye waunganishe na Kamati ya Bajeti.

“Lakini waheshimiwa wabunge naomba niseme si tabia njema hasa kwetu sisi wabunge kuzua maneno, unajua maneno ya uzushi na uongo ni mbaya sana katika jamii yetu wenyewe, hii inaweza kuwa kwa wabunge lakini pia hata waandishi wa habari,” alisema.

Spika alisema katika sheria za utungaji wa sheria, kifungu cha usikilizwaji kwa umma ni rasmi na kwamba hakuna muswada wowote unaopita bila kuwashirikisha wanaohusika na matumizi ya miswada hiyo.

Kuhusu wafanyabiashara kufanya ushawishi kwa kamati ya bajeti ili misamaha ya kodi isifutwe, alisema: “Duniani kote ushawishi upo, washawishi wapo, maana yamezuka maneno wafanyabiashara wamewashika kamati ya bajeti, hayo ni maneno ya uzushi kwa sababu hata wewe mbunge  mmoja unaweza kushawishiwa.

“Sasa busara ya kila ushawishi wewe unayeshawishiwa si kwamba unaunganisha kila kitu unaondoka nacho unakuja kurundika humu ndani, hiyo si busara, tumia mawazo yako kuweza kuchanganua kinachofaa kwa wananchi.”

Spika alisema katika kufanya kazi Bunge linataka kuimarisha ufanyaji kazi wa wabunge ambao si wataalamu wa kila kitu, bali kuna wataalamu sehemu nyingine ambao wanaweza kufaa zaidi.

“Kwa hiyo tunasema haya hata ikibidi tunatafuta wataalamu, tuache tabia hii,  inatufanya tunakuwa wadogo mno, tunakuwa wafinyu, kwa hiyo hata magazeti yanapoandika kamati imekula fedha, nani kawapa fedha na kama wapo vyombo vinavyohusika vipo wewe kama unajua kwa nini usiwaambie fulani anachukua fedha, hatujengi nchi kwa majungu, tuwe waangalifu na midomo yetu, mahali popote panapoendeshwa na majungu pamepungukiwa,” alisema.

Pamoja na uamuzi huo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alishangaa hatua hiyo ya Spika kuahirisha miswada hiyo ambapo alisema haoni sababu ya miswada hiyo kucheleweshwa wakati imepitia hatua zote.

Kuhusu kuahirishwa kwa miswada hiyo, alisema suala hilo lilipitia kwenye kikao cha makatibu wakuu wote wa wizara zote na kila Katibu Mkuu alishirikisha wataalamu na wadau wa sekta ya wizara yake, pia lilikwenda kwenye Baraza la Mawaziri ambalo kiongozi wake ni Rais.

“Hili ni jambo ambalo tangu tuje hapa bungeni wabunge wote, kamati zote, ripoti zote za kambi ya upinzani, ripoti zote Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, sioni jambo ambalo wabunge hatulijui kuhusu muswada wa VAT,” alisema.

Muswada huo ulikuwa uwasilishwe bungeni jana na kujadiliwa kwa siku mbili, yaani Julai mosi hadi Julai 2, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles