KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
MAOMBI ya kupinga kushikiliwa kwa ndege ya Tanzania, Airbus nchini Afrika Kusini yanatarajiwa kusikilizwa leo na Mahakama Kuu nchini humo.
Akizungumzia kesi hiyo jana Wakili Mkuu wa Serikali Msaidizi, DK Ally Possi alisema mawakili kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, watashirikiana na mawakili wa Afrika Kusini katika maombi ya kupinga kushikiliwa kwa ndege hiyo.
“Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wanasimamia suala hilo kuhakikisha ndege hiyo inaachiwa,”alisema.
Ndege hiyo ilishikiliwa kutokana na maombi namba 28/994/2019 yaliyowasilishwa na mwombaji Hermanus Steyn kupitia ofisi ya uwakili ya Werksmans iliyopo nchini humo.
Maombi hayo ya kusikilizwa upande mmoja yaliwalishwa Agosti 21 mwaka huu dhidi ya Serikali ya Tanzania, Uwanja Ndege wa Afrika Kusini, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Afrika Kusini, Kampuni ya Ndege Tanzania, Sibusis Nkabinde, Mr Kgomotso Molefi na Mr Patrick Sithole.
Katika maombi hayo kuliambatanishwa na kiapo, kilichoapwa na na Martin Richard Steyn na Bianka Pretorius wakisapoti maombi ya kushikilia ndege kwa sababu mdai anadai Serikali ya Tanzania Dola za Marekani 36,375,672.81.
Mahakama ilisikiliza maombi hayo upande mmoja na tarehe hiyo hiyo yaliyowasilishwa na kukubali hoja za mwombaji na kuamuru ndege ikamatwe.
Mwaka 2010 mbele ya Jaji Mstaafu Josephat Manckanja, mdai alikuwa anadai fidia ya shamba lake jumla ya dola za Marekani milioni 36.
Mahakama ilikataa, pande zote mbili wakaketi kwa ajili ya makubaliano wakifikia makubaliano ya kulipa dola za Marekani milioni 30.
Baada ya makubaliano hayo Serikali ya Tanzania ilianza kulipa na ilishalipa kiasi kikubwa cha fedha.
Pamoja na kuwa tayari malipo yalishafanyika kwa kiasi kikubwa, mdai katika maombi yake anadai kiwango kile kile cha awali cha zaidi ya dola za Marekani milioni 36 kilichokuwepo kabla ya makubaliano.