24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wakili anayepinga Mwambe kuendelea ubunge akwaa kisiki

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

WAKILI Paul Kaunda anayepinga kauli ya Spika wa Bunge Job Ndugai kumtambua Cecil Mwambe kuwa bado ni mbunge, amegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu kutupa maombi yake kwa sababu alikosea kufungua shauri la kikatiba.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa jana mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Issa Maige.

Wengine ni Jaji Stephen Magoiga na Jaji Seif Kulita.

Akisoma uamuzi wa jopo hilo, Jaji Maige alisema pamoja na mambo mengine, mleta maombi alidai maelezo ya Spika kutamka kwamba anamtambua Mwambe kuwa ni mbunge wa Ndanda pamoja na kwamba alijivua uanachama Chadema yanakwenda kinyume na Katiba.

Alisema katika maombi yake, mwombaji alidai kwamba Mwambe kwa kujivua uanachama si Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Jaji Maige alisema maombi hayo yalifunguliwa chini ya Ibara ya 26.

Akisoma uamuzi, Jaji Maige alisema mahakama haikubaliani na hoja tatu, inakubali hoja moja kwamba mleta maombi alikosea kufungua shauri kwa kutumia Ibara 26 ya Katiba.

Alisema maombi yaliyofikishwa mahakamani si ya kikatiba, bali yanahusu utaratibu, hivyo hakupaswa kufungua shauri la kikatiba badala yake angefungua la kawaida.

“Maneno yaliyozungumzwa na Spika yalikuwa ya kaiwada katika utaratibu wa utendaji kazi wake,” alisema Jaji Maige.

Alisema kwamba mleta maombi alipaswa kutumia Ibara ya 83 kueleza malalamiko yake mahakamani.

Ibara hiyo inasema: “(1) Kila shauri kwa ajili ya kupata uamuzi juu ya suala- (a) kama uchaguzi au uteuzi wa mtu yeyote kuwa mbunge ulikuwa halali au sivyo; au

(b) kama mbunge amekoma kuwa mbunge na kiti chake katika Bunge ki wazi au hapana, litafunguliwa na kusikilizwa kwanza katika Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii. 

“ (2) Iwapo Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake  kwa mujibu wa masharti ya ibra ya 41(3) ya Katiba hii imemtangaza mbunge yeyote kwamba amechaguliwa kuwa Rais, basi hakuna mahakama wala chombo chochote kingine kitakachochunguza zaidi suala lolote linalohusu kiti cha mbunge  huyo kuwa wazi.”

Awali jopo la mawakili wa Serikali, likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vicent Tango, waliwasilisha hoja nne za pingamizi wakidai mdai hana haki ya kisheria kupewa nafuu anazoziomba katika shauri hilo na kwamba hati ya kiapo kinachounga mkono maombi hayo ina kasoro za kisheria ambazo haziwezi kurekebishika.

Serikali inadai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kusikiliza shauri hilo na kutoa nafuu zinazoombwa kwa mujibu wa Ibara ya 100 (1) ya Katiba ya Nchi na kifungu cha 3 cha Sheria ya Bunge ya Haki Kinga na Mamlaka na kwamba shauri hilo halina maana kwani ni la usumbufu tu.

Vilevile Serikali inadai kuwa shauri hilo halistahili kwa kuwa linakinzana na Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi, pamoja na Ibara ya 26(2) ya Katiba ya nchi.

Pamoja na pingamizi hilo, pia Serikali katika majibu yake inadai kuwa Mwambe bado ni mbunge halali wa Ndanda kwa mujibu wa Katiba na sheria nyingine za nchi na anastahili stahiki zote kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazotumika kusimamia masuala ya Bunge.

Hivyo Serikali inadai Ibara iliyotumika kufungua shauri hilo hakikustahili  na kwamba Spika hajavunja sharti lolote la Katiba ya nchi kama inavyodaiwa, na hivyo inamtaka mdai kuthibitisha madai yake.

Hoja zote hazikukubaliwa na jopo hilo isipokuwa hoja moja kwamba mwombaji alipaswa kutumia Ibara ya 83 badala ya Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles