21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

WAKENYA WAHOFIA KUWAFUNGULIA WAGENI MIPAKA

NAIROBI, KENYA


AGIZO la Rais Uhuru Kenyatta la kuwafungulia raia wa mataifa ya Afrika milango ya kuingia Kenya kuishi, kumiliki mali na kufanyabiashara, limepokewa kwa hisia tofauti na Wakenya.

Baadhi ya wadadisi wanasema linaweza kuchangia kustawisha uchumi wa Kenya, huku wengine wakionya ni hatari kwa usalama wa taifa.

Akihutubia umati wakati wa sherehe ya kuapishwa kuhudumu kwa kipindi cha pili madarakani, Rais Kenyatta alisema urahisishaji wa masuala ya uhamiaji utakuza biashara barani Afrika.

“Raia wa mataifa ya Afrika watakuwa wakipokea viza mipakani na katika viwanja vya ndege. Hatufanyi hivi tukitarajia chochote kutoka nchi zao,” alisema Rais Kenyatta.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, Francis Atwoli, alikuwa wa kwanza kupongeza hatua hiyo akisema itafanya marais wa nchi za Afrika kufuata nyayo za Rais Kenyatta.

“Mimi binafsi nilifanya juhudi za kuwashawishi marais wa nchi za Afrika Mashariki kuruhusu raia wa nchi zao kutembelea nchi wanachama bila vikwazo,” alisema Atwoli.

Aidha Rais Kenyatta, alilegeza masharti ya raia wa nchi za Afrika Mashariki kuishi Kenya akisema watakachohitajika ni kitambulisho tu.

“Kenya inajivunia kuwa mwanachama wa jamii ya kimataifa na tutaendelea kufanya bidii. Tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu wa kibiashara,” alisema.

Lakini wanaokosoa hatua hiyo wanasema ni tisho kwa usalama, hasa kipindi hiki ambacho ugaidi unaisumbua dunia.

Wanasema maofisa wa usalama watahitajika kukaa chonjo kuhakikisha wahalifu na magaidi hawatumii fursa hiyo kupenya mipakani na kuendeleza vitendo vyao.

Kwa mujibu wa Demitrio Aseka, mtaalamu wa masuala ya uhamiaji, agizo la rais litaathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya kijamii, kiuchumi na usalama wa Kenya.

“Kuna gharama ya kufungua mipaka ya nchi. Kwa hakika siku hizi nchi zinaendelea kuimarisha usalama mipakani,” alisema Aseka.

Mtaalamu wa masuala ya usalama, Simiyu Werunga, alisema pamoja na kuwa kauli ya rais inaonekana kuvutia kisiasa, inaweza kuathiri usalama wa nchi ambayo ina rasilimali chache.

Werunga alisema kutokana na ukweli kwamba Kenya inazungukwa na mataifa yanayokumbwa na vurugu kama Somalia na Sudan Kusini, kufungua mipaka au kulegeza masharti ya uhamiaji kunapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa.

“Bila shaka kuna changamoto za kiusalama. Kenya ina majirani ambao ni kitovu cha ugaidi,” alisema.

Hofu ya wataalamu wa usalama ni kwamba wahalifu wa kimataifa wanaweza kutumia Kenya kupitishia dawa za kulevya, ulanguzi wa binadamu, fedha na bidhaa bandia.

Hata hivyo, wanauchumi wanasema kuwa hatua hiyo inaweza kustawisha Kenya kiuchumi na kijamii iwapo mataifa mengine ya Afrika yatawafungulia Wakenya mipaka yao.

“Vikwazo vya uhamiaji vimekuwa kizingiti kwa maendeleo barani Afrika. Hata hivyo kila hatua inafaa kuchukuliwa kulinda uchumi na usalama wa nchi inayofungua mipaka ili wageni wasipore utajiri wake,” alieleza Raju Shah, mtaalamu wa masuala ya uchumi.

Mkurugenzi wa Uhamiaji, Gordon Kihalangwa, amesema kabla ya uamuzi wa kuwafungulia mipaka raia wa nchi za Afrika, masuala mengi yalizingatiwa.

Hata hivyo, alionekana kukiri kwamba kuna haja ya kulinda usalama wa ndani wa Kenya, akisema wageni wote watakaguliwa vikali kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

Shah alisema Kenya ina watu walio na ujuzi katika sekta mbalimbali kuliko mataifa mengine, ambao hawana kazi, na kuwaruhusu raia wa kigeni kufanya kazi nchini kutawanyima ajira na rasilimali haba zilizopo.

Hata hivyo, alisema kulegeza masharti kwa wawekezaji pekee ni sawa kwa sababu watabuni nafasi za kazi kwa Wakenya.

“Serikali inafaa kulenga wawekezaji pekee. Kuruhusu raia wa kigeni kuingia nchini kufanya kazi ilhali theluthi tatu za Wakenya hawana kazi ni mzaha. Ni kibaya zaidi kuruhusu wageni kumiliki ardhi wakati ambao kuna Wakenya wengi wasiomiliki,” alisema Aseka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles