Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM
WAKAZI wa Mtaa wa Kunguru, Kata ya Goba, Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam wameomba mamlaka kuwabadilishia jina la mtaa wao kwani lililopo haliwafai.
Wakizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa wananchi na Kampuni ya Upangaji na Upimaji Makazi (HUSEA), uliofanyika Shule ya Upili ya Mtakatifu Joseph iliyopo Goba, wakazi hao walisema jina la Kunguru na tabia ya ndege huyo za wizi na uchafu, linaupa taswira mbaya mtaa wao.
Kilio cha wananchi hao pia kilisikilizwa na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob aliyetakiwa awasaidie kubadilisha jina hilo. Hata hivyo wananchi hao hawakutaja jina jipya ambalo wanalitaka.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Meya Jacob alisema hakuna ugumu kwenye kubadili jina ikiwa wengi wataridhia, huku akiwapa utaratibu wa kufuata waweze kutimiza matakwa yao.
Alisema wanachotakiwa kukifanya ni kukusanya sahihi zisizopungua nusu ya wakazi wa mtaa mzima na waandike barua kwa halmashauri kuomba kubadilisha jina na kutaja jipya wanalolipendekeza.