24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wakandarasi watakaochelewesha miradi ya maji kutoongezewa muda

Na Mohamed Saif, Mwanza

Serikali haitowaongezea muda wakandarasi watakaoshindwa kukamilisha miradi ya maji kwa wakati na badala yake watanyang’anywa na itatekelezwa na wataalam wa ndani.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema hayo Februari 24, 2021 kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza.

“Wakandarasi ambao wanachelewesha miradi tutafuatilia ukomo wa mikataba yao na hatutaruhusu muda wa nyongeza labda tu kuwe na sababu za msingi zilizosababisha mradi kuchelewa,” alisisitiza Naibu Waziri Mahundi.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (katikati) kwenye mradi wa ujenzi wa tenki la maji la Buswelu, Wilayani Ilemela. Kushoto ni Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Severine Lalika

Alisisitiza kwamba Serikali haitomvumilia Mkandarasi yoyote mzembe na kwamba miradi itakayoshindwa kukamilika kwa wakati kama ilivyo kwenye mkataba itakamilishwa kwa utaratibu wa force account.

“Bahati nzuri tunao wataalam wazuri sasa mkandarasi atakayekwenda kinyume na mkataba ikiwa ni pamoja na kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati, tunampokonya mradi na tunatekeleza wenyewe,” alisisitiza Mhandisi Mahundi.

Alisema inasikitisha kuona mkandarasi anashindwa kukamilisha mradi aliyokabidhiwa licha ya kwamba amepewa fedha kama ilivyo kwenye mikataba ya utekelezaji wake na alisisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haipo tayari kuendelea kufanya kazi na mkandarasi wa namna hiyo.

“Serikali hii ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni ya vitendo, suala la mkandarasi kuongezewa muda bila sababu ya msingi hiyo haikubaliki, kwanini mkandarasi uwe kikwazo kwenye kutekeleza miradi licha ya kwamba unalipwa fedha yako kwa wakati, hii sio sawa,” alisisitiza Mahundi.

Aidha, Naibu Waziri Mahundi alibainisha kwamba Serikali  imeazimia ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa majisafi na salama maeneo ya mijini uwe zaidi ya asilimia 95 na maeneo ya vijijini uwe zaidi ya asilimia 85.

Alisisitiza kwamba dhamira ni kumtua mama ndoo kichwani na kwamba hilo litafanyika kwa kuhakikisha huduma ya maji inafikishwa katika kila kaya na siyo kuishia kwenye vituo vya kuchotea maji maarufu kama vioski.

“Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli imejipambanua katika kumkomboa mwanamke na hili litafanyika kwa kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani kwa kumfikishia bomba la maji nyumbani kwake,” alifafanua Naibu Waziri.

Akizungumzia miradi ambayo kwa muda mrefu imekua ikisuasua ama miradi kichefuchefu hususan kwenye maeneo ya pembezoni ambayo ilikabidhiwa  kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),  Mhandisi Mahundi alithibitisha kuwa utekelezwaji wake unakwenda vizuri na baadhi yake itakazinduliwa mnamo mwezi Machi mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maji.

Aidha, Naibu Waziri Mahundi aliipongeza ushirikiano baina ya Serikali za Wilaya za Nyamagana na Ilemela na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na RUWASA Mkoa wa Mwanza na kuzitaka taasisi zingine kwenye Sekta ya Maji kuiga mfano huo.

“Lazima wataalam Sekta ya Maji tuwe na utamaduni wa kujenga mahusiano na Ofisi za Serikali kwenye maeneo ya miradi. Ushirikiano niliyouona hapa umenifurahisha na wengine muige kutoka hapa,” alisisitiza Mhandisi Mahundi.

Naibu Waziri Mahundi yupo Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku mbili ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji na ametembelea ujenzi wa mradi wa tenki wa Sahwa, Wilayani Nyamagana na mradi wa ujenzi wa tenki wa Buswelu Wilayani Ilemela ili kujidhirisha na hatua iliyofikiwa sambamba na kuzungumza na wasimamizi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles