Na Derick Milton,
WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) imeendelea na uhakiki wa mizani kwa makampuni ya kununua pamba mkoani Simiyu katika kuhakikisha wakulima wa zao hilo hawaibiwi.
Vilevile imekagua mizani za wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa mazao ya nafaka na kutoa elimu.
Meneja wa WMA mkoani Simiyu, Augustine Maziku, alisema mizani 1,500 tayari imekaguliwa kutoka makampuni hayo na wafanyabishara.
Maziku alisema hatua hiyo ya kutoa elimu na uhakiki wa mizani inayotumika kununulia pamba na mazao mbalimbali linaendelea kwa kwa wananchi wote ambao wana maduka ya kuuza nafaka.
Alisema wakala inatarajia kutembelea vijiji vyote mkoani humo kutoa elimu na kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwa wanunuzi wa pamba.
Hatua hiyo ina lengo la kuona kama mizani iliyopimwa na ikaonekana ni sahihi inaendelea kununua pamba ya wakulima kwa vipimo sahihi.
“Kuna wakulima wanalalamikiwa kuweka maji, kokoto na mchanga kwenye pamba kwa ajili ya kuongeza uzito.
“Tunawataka waache tabia hiyo mara moja, sheria ya vipimo ipo na inafanya kazi kwa pande zote mbili muuzaji na mnunuzi, wote kwa pamoja hawatakiwi kufanya udanganyifu wowote katika biashara,” alisema Maziku.
Meneja wa WMA makao makuu, Richard Kadege alisema lengo kuu la kukagua mizani na kutoa elimu kwa ajili ya kumlinda mlaji.
Alisema hatua hiyo itamwezesha mlaji apate faida na thamani ya kile alichozalisha na siyo kupunjwa na wafanyabiashara wajanjawajanja.