YANGA YAMWAMGUKIA ALIYEKUWA MWENYEKITI WAO

0
472

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

UONGOZI wa Yanga kupitia kamati yake maalumu, umemwangukia Mwenyekiti wa klabu hiyo na kumwomba afikirie upya uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi hiyo, baada ya klabu kudaiwa kukumbwa na hali mbaya ya kiuchumi.

Mei mwaka huu kigogo huyo aliandika barua ya kujiuzulu nafasi yake kwa madai kwamba ametingwa na majukumu binafsi, hivyo ametoa fursa kwa Wanayanga wengine kupokea kijiti cha kuiongoza klabu hiyo kongwe nchini.

Barua hiyo ilipokewa na uongozi wa Yanga na kujadiliwa kabla ya viongozi wa matawi ya klabu hiyo kukutana hivi karibuni na kukubaliana kuunda kamati maalumu ambayo tayari imewasilisha ombi kwa Mwenyekiti huyo kumwomba afute uamuzi wake.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Salum Mkemi, alisema baada ya kuwasilisha ombi hilo sasa wanasubiri jibu kutoka kwa milionea huyo  kama atakubali kubadili uamuzi wake wa kutaka kujiuzulu.

“Hakuna mgogoro wowote ndani ya Yanga ambao umesababisha Mwenyekiti atangaze  kujiuzulu nafasi yake, bali uamuzi huo aliufanya mwenyewe bila ya kushinikizwa na mtu yeyote.

“Kwa kuthibitisha kwamba Yanga tupo shwari, kwa pamoja tumekubaliana kupeleka ombi letu la kumwomba mwenyekiti kufikiria upya uamuzi wake, hivyo itakuwa ni hiyari yake kukubaliana na ombi letu,” alisema Mkemi.

Inadaiwa kwamba uongozi wa Yanga umefikia uamuzi wa kumwangukia mwenyekiti wao kutokana na kubanwa na hali ngumu ya kiuchumi tangu alipotangaza kujiondoa, hasa katika suala zima la usajili wa wachezaji kwa maandalizi ya msimu ujao wa ligi.

Akizungumzia kuhusu usajili wa kimya kimya unaofanywa na klabu hiyo, Mkemi alisema hawatengenezi kikosi kibaya msimu ujao bali wanataka kuboresha maeneo ambayo Kocha Mkuu, George Lwandamina, aliona kuna mapungufu.

Aidha, Mkemi aliongeza kuwa klabu imefikia azimio la kuwabakiza nyota wake wote ambao wanawategemea kuwa watatoa mchango mkubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao na  michuano ya kimataifa mwakani.

“Tetesi zilizozagaa kwamba tumeachana na wachezaji wetu ambao ni tegemeo kwenye timu zinatengenezwa tu, malengo yetu ni kuwabakisha nyota wote muhimu ambao walisaidia katika mafanikio ya kutetea ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya tatu mfululizo,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here