28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WAKALA WA MAJENGO (TBA) APEWA NYUMBA ZA CDA

Na ANGELA MSIMBIRA – TAMISEMI

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mussa Iyombe, amesema zaidi ya kaya 438 za watumishi wa umma watakaohamia Dodoma na wenye sifa  ya kupatiwa nyumba na Serikali watakuwa na uhakika wa kupata nyumba zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).

Akikabidhi nyumba zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu kwa  Wakala wa Majengo (TBA), Iyombe alisema nyumba hizo zitakuwa maalumu kwa watumishi wenye sifa kulingana na miundo ya kiutumishi.

“Nyumba  ambazo zinakabidhiwa kwa Wakala wa Majengo ni nyumba za kuishi ambazo awali zilimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu na kuhamishiwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma,” alisema Iyombe.

Kutokana na hali hiyo, alisema baada ya kuvunjwa kwa CDA, iliagizwa  kuwa watumishi  wote waliokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)  kupangiwa kazi  kwenye Ofisi za Serikali na kipaumbele cha kwanza kilikuwa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuchagua watumishi wanaomfaa kwa ajili ya kuendeleza kazi zilizokuwa zikifanywa na CDA.

Alisema mali zilizokuwa zikimilikiwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu yakiwemo majengo ya kibiashara kama vile  maduka na  ofisi zimeelekezwa zibaki chini ya  Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, lakini majengo ya makazi  yakabidhiwe kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

“Hatuna lengo la kuidhohofisha Manispaa ya Dodoma lakini Serikali  inaangalia wanafaidika nini na nyumba hizo wakati majengo yote ya Serikali yanatakiwa kuwa chini ya Wakala wa Majengo Tanzania.

“Na wakati huo huo watumishi wote wa Serikali wanahamia Dodoma  na hawana maeneo ya kuishi, nyumba zipo zilizokuwa zinamilikiwa na CDA zinapangishwa kwa wapangaji ambao hawalipi pango za nyumba kwa wakati,” alisema Iyombe.

Akifafanua zaidi alisema majengo yaliyopo ni 141, kati ya hayo kuna magorofa 45 hivyo familia ambazo zinaweza kuingia katika majengo hayo ni kaya 438, hivyo matarajio ya Serikali ni kwamba watumishi 438 wenye sifa ya kupatiwa nyumba waliopo Dar es Salaam watapata makazi hapa Dodoma.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, alisema wamepokea maelekezo ya Serikali ya kukabidhi nyumba za makazi kwa Wakala wa Majengo Tanzania kwa kuwa Dodoma sasa ni Makao Makuu ya Nchi.

‘‘Kumekuwapo  na changamoto ya makazi  kwa watumishi wanaohamia Dodoma, lakini nyumba zinazokabidhiwa  zipo katika hali ya matumizi na nyingine zinahitaji ukarabati ambao tunadhani wenzetu wa TBA wataendelea nao,” alisema Kunambi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles