28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wajibu wa kumlinda mtoto ni wetu sote  

masajuNa Kulwa Mzee, Dar es Salaam

HABARI wasomaji wa Haki Hainunuliwi, katika safu yetu wiki hii tutazungumzia unyanyasi wanaofanyiwa watoto.

Sote tunakubaliana kwamba watoto wana haki ya kulindwa, hawastahili kunyanyaswa.

Kwa kufahamu hilo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Sheria na Katiba, walimuandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakitaka sheria ya mtoto ifanyiwe mabadiliko kwani inakinzana na juhudi za Serikali za kumlinda mtoto.

Takwimu za ubakaji zinaeleza kwamba matukio ya mwaka 2015 yameongezeka mara tano ya matukio yaliyotokea mwaka 2014.

Takwimu za Polisi zinaonyesha mwaka 2014 matukio ya ubakaji watoto yalikuwa 422, mwaka 2015 yaliongezeka na kufikia 2,358, hali si nzuri ni zaidi ya mara tano ya matukio ya mwaka 2014.

Takwimu zinasema matukio ya ubakaji watoto Januari hadi Machi 2016 yalikuwa 1765, hii inaonyesha mwishoni mwa mwaka huu matukio ya ubakaji kwa watoto yatakuwa mengi zaidi.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inasema watoto wa kike watatu kati ya 10 walishawahi kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono mara moja kabla ya kufikia umri wa miaka 18.

Kwa watoto wa kiume, mmoja kati ya saba walishafanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, kwa vitendo vya ukatili, watoto wa kike wanne kati ya 10 wameshafanyiwa vitendo vya ukatili na watoto wa kiume watatu kati ya 10 walifanyiwa ukatili kabla ya umri wa miaka 18.

Wizara inasema asilimia 49 ya watoto wanafanyiwa ukatili nyumbani sehemu ambayo wanatakiwa kuona ni salama kwao huku asilimia 23 wakifanyiwa ukatili wanavyotoka shuleni na asilimia 15 hufanyiwa shuleni.

Katika mazingira hayo ni wajibu wa kila mmoja kumlinda mtoto kwani takwimu zinaonyesha ukatili unafanyika hata katika mazingira ya nyumbani anakoishi.

Ni ushauri unaotakiwa kupewa kipaumbele kwamba wazazi ama walezi wawe makini hasa katika kuwalaza watoto na ndugu katika chumba kimoja.

Ukatili unaonekana wazi unafanywa na watu tunaowajua hivyo aibu ama huruma ya kuchukua tahadhari inaweza kusababisha watoto wakadhurika kwa kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji.

Wataalamu wanaelekeza wazazi wasiruhusu mtoto wa kike wala wa kiume kulala na ndugu mwanamume chumbani.

Hilo linaweza likaonekana kama linamnyanyapaa mgeni lakini tunatakiwa wote kuelewa kuwa si kila mgeni anaweza kuwa mstaarabu anayejali haki za watoto.

Tumekuwa tukishuhudia matukio mengi yanayofanywa na watu wenye akili timamu, maswali mengi tunajiuliza bila majibu hivyo hakuna namna zaidi ya kuchukua tahadhari kwa kila mtu ili kumlinda mtoto.

Kila kukicha kunaibuka watu wenye roho za kinyama, wanawaharibu watoto wadogo, wanawakatisha masomo kwa kuwabaka na wengine kuwarubuni kwa fedha.

Ili kukomesha unyanyasaji huu kila mmoja ana wajibu wa kumlinda mtoto bila kujali ni wake ama si wake, tunatakiwa kujenga dhana kwamba mtoto hata kama akiwa wa mwezako ni wako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles