33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 13, 2024

Contact us: [email protected]

WAJAWAZITO WAPANDA MAGARI YA MKAA

NA GUSTAPHU HAULE-PWANI

 

WAJAWAZITO wa Kata ya Kibindu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, wanalazimika kupanda magari ya mkaa kwa ajili ya kutafuta huduma ya uzazi katika vituo vya afya vilivyopo mbali na maeneo yao kutokana na ukosefu wa magari ya wagonjwa (ambulance) katika kata hiyo.

Diwani wa Kata hiyo, Ramadhani Mkufya (CCM), aliibua hoja hiyo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika juzi mjini Lugoba, ambapo alisema wajawazito na wagonjwa wengine katika kata yake wamekuwa wakikabiliwa na adha hiyo kwa muda mrefu.

Kutokana na hali hiyo, Mkufya aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Edes Lukoa, kuhakikisha inapeleka gari la wagonjwa katika kata hiyo ili kuweza kuokoa maisha ya wananchi wake hususani wajawazito.

“Kibindu hakuna gari la wagonjwa badala yake wagonjwa wakiwemo wajawazito wamekuwa wakipanda magari yanayobeba mkaa  kwa ajili ya kufuata huduma ya afya sehemu mbalimbali, hivyo naiomba Halmashauri isaidie kutatua jambo hili kwa haraka,” alisema Mkufya.

Alisema  kama halmashauri haina uwezo wa kununua magari mapya, ni vyema kwa sasa wakaweka jitihada za kutengeneza magari mabovu yaliyopo katika Halmashauri hiyo ili yaweze kuwasaidia wananchi hao wakati taratibu za kununua magari mapya zikiendelea kufanyika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Edes Lukoa, alisema kilio cha diwani huyo ni sahihi na kwamba halmashauri itatumia mapato yake ya ndani katika kumaliza tatizo hilo.

Alisema halmashauri inatengeneza ambulance moja mbovu iliyokuwa ikifanya kazi katika maeneo ya Kwamrohombo na kwamba inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na itapelekwa katika Kata hiyo.

Alisema Kata ya Kibindu inahitaji  gari la wagonjwa, kwa sababu wajawazito 30 hujifungua ndani ya mwezi mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles