25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

WAJASIRIAMALI WATUMIE SOKO LA HISA KUKUZA MTAJI

NA GEORGE MSHANA,

WAJASIRIAMALI wadogo na wa kati wachangamkie fursa ya kujiunga na soko la hisa, lengo likiwa ni kukuza mitaji ya wajasiriamali wadogo na wa kati yaani Enterprise Growth Market (EGM), ili waweze kukuza mtaji wao na kuongeza mchango wao katika pato la taifa na kutoa nafasi za ajira.

Hayo yamesemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Moremi Marwa, katika jarida la soko la hisa linalotoka kila baada ya miezi mitatu.

“Wajasiriamali wadogo na wa kati wawe na malengo ya muda mrefu, hasa katika kipindi hiki ambapo mikopo kwa kilimo na viwanda vidogo vya uzalishaji mali kutoka kwenye benki za biashara inapungua. Hali hii inaweza kuendelea hasa katika kipindi ambacho riba na hati fungani za Serikali zinapungua kutokana na matatizo ya kifedha yaliyopo kwenye benki za biashara.

Changamoto hii inaweza kusababisha mikopo inayotolewa na mabenki kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kupungua na hivyo njia pekee ya kuongeza mtaji wake ni kwa kujiunga na soko la hisa ili kukuza mtaji wake,” alisema Marwa.

Soko la hisa linaweza likawa ndiyo njia mbadala ambayo wajasiriamali wanaweza kuitumia kukuza mitaji yao, hasa ukizingatia kwamba uwezekano wa wao kuweza kupata mkopo kutoka kwenye mabenki ya biashara ambayo riba yake ni kubwa na masharti yake ni magumu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kuweza kumudu, ni mdogo. Hivyo, soko la hisa linaweza likawasaidia kukua na kupanuka kibiashara.

Vile vile, masharti ya kujiunga katika soko la hisa ambalo lengo lake ni kukuza mitaji ya wajasiriamali wadogo na wa kati EGM, ni nafuu kuliko yale ya kujiunga katika soko kuu la soko la hisa ambapo makampuni yanayojiunga hapo yanatakiwa kuwa yanafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu na miwili kati ya hiyo wanatakiwa wawe wamepata faida. Makampuni yanatakiwa pia kuonyesha ni jinsi gani watatoa gawio kwa wanahisa wake na iwe na mtaji wa Sh bilioni moja. Pia inatakiwa iwe hesabu zake zimekaguliwa.

Makampuni yanayotaka kujiunga na soko la hisa ambalo lengo lake ni kukuza mitaji ya wajasiriamali wadogo na wa kati, yanatakiwa kila moja kuuza asilimia 10 ya hisa zake na kuwa na wanahisa angalau 100. Kwenye Soko Kuu la Soko la Hisa, makampuni yanayotaka kujiunga yanatakiwa kuuza asilimia 25 ya hisa zao na kuwa na wanahisa 1,000.

Katika soko la hisa, wajasiriamali wadogo na wa kati wana fursa ya kupanua wigo wa kupata vyanzo vya mapato kupitia uuzaji wa hisa zao na hivyo kupata fedha zitakazokuza mtaji wao.

“Wajasiriamali wadogo na wa kati waliojiunga na soko la hisa, wanaweza kusaidia kuwa na mahusiano mazuri kati ya wajasiriamali wadogo na wa kati na mabenki. Mjasiriamali ambaye hisa zake zimeorodheshwa kwenye soko la hisa, anaonekana kwamba anaweza kukopesheka na mabenki kuliko mjasiriamali mdogo na wa kati ambaye hisa zake hazijaorodheshwa kwenye soko la hisa,” alisema.

Duniani kote Serikali na masoko ya mitaji wanatambua mchango wa wajasiriamali wadogo na wa kati katika ukuaji wa uchumi na utengenezaji wa nafasi za ajira, ndio maana hata masoko ya hisa yaliyoendelea yana sehemu ya soko la hisa, ambapo wajasiriamali wadogo na wa kati wamepewa fursa ya kujiunga na hatimaye kukuza mitaji yao.   Hii inasaidia kuweza kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi na kutengeneza nafasi za ajira na hivyo kuchangia katika jitihada za Serikali za kupunguza umasikini. 

Katika soko la hisa la Dar es Salaam, kuna makampuni matano ambayo yanawajumuisha watu 250,000. Kukua kwa mtaji ni takriban Sh bilioni 50 kupitia toleo la awali (IPO) na mtaji uliopo katika soko ni bilioni121. Wajasiriamali wadogo na wa kati wanakadiriwa kuwa milioni tano hapa nchini na wanaajiri watu wengi sana kiasi cha asilimia 45 katika sekta isiyo rasmi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles