28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

TANZANIA KUTUMIA WAFUNGWA KUJENGA RELI MWENDOKASI

Na Mwandishi Wetu,

SERIKALI ya Tanzania imefafanua kuwa ujenzi wa reli ya mwendokasi toka  Dar es Salaam hadi Morogoro, utatumia fedha zake za ndani na ziko kwenye bajeti yake na si mkopo kama wengi wanavyofikiri.

Rais John Maguguli alitoa ufafanuzi huo kwenye sherehe ya kumwapisha Mkuu mpya wa Majeshi, Generali Venance Mabeyo, Ikulu mjini Dar es Salaam.

Alisema Treni ya kisasa itakayotoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambayo itakuwa inatumia umeme, reli yake itajengwa kwa kiasi cha Sh trilioni 2 ambazo ni fedha za Watanzania na si fedha za Waturuki kama ilivyoripotiwa  na baadhi ya vyombo vya habari wakirejea Kampuni ya Bloomberg ya Marekani.

Aliendelea kusema kuwa reli itakayojengwa itakuwa na umbali wa kilomita 300, ikiwa njia kuu na zile za kupishana  pamoja na matoleo kwa ajili ya kubebea mzigo.

“Hii reli ambayo tunapanga kuijenga, itakuwa ya kisasa zaidi kwani itatumia umeme, sasa kuna watu wanadhani fedha za ujenzi wa reli hiyo ni za Waturuki, hapana kwa asilimia mia ni fedha za Serikali,” alisema Rais Magufuli na kuthibitisha kuwa muda wa ujenzi utakuwa miezi 30 na itakuwa na uwezo wa kukimbia kwa mwendo wa kilomita 180 kwa saa, tofauti na treni ya sasa hivi ambayo inakimbia kwa mwendo wa kilomita kati ya 30 na 50 kwa saa,” alisema.

Akilinganisha reli hiyo na zile zinazojengwa  nchi jirani za Ethiopia na Kenya, kuwa  tofauti na reli zinazojengwa katika nchi hizo ambazo ‘excel’ zake zina uwezo wa kubeba tani 25, reli hiyo ya kisasa ‘excel’ yake itakuwa na uwezo wa kubeba tani 38 na hivyo kutoa  nafasi kubwa ya kubeba na kusafirisha mzigo.

Ripoti zinaonesha kuwa reli hiyo mpya ina uwezo wa kubeba tani milioni 17 kwa mwaka.

Rais alisisitiza umuhimu wa reli hiyo kujengwa na kudai nguvu na rasilimali zote za Serikali zitumike ili kupata mafanikio, ikiwa ni pamoja na kutumia wafungwa ili kupunguza gharama za ujenzi na kutumia kikamilifu rasilimali watu hiyo.

Dk. Magufuli akaagiza kuwa wafungwa washiriki kwenye ujenzi wa reli hiyo katika nguvu kazi, ikiwemo kuponda kokoto na kusema: “Waponde kokoto, wasukume mawe, wakitoka gerezani wawe safi na wasifanye mabaya tena.”

Rais Magufuli alitaka wafungwa wafanye kazi katika misingi ya kuzalisha mali na si kukaa tu wanakula kwa kisingizio kuwa wamefungwa kifungo cha muda mrefu. Alisema hao waliofungwa miaka mingi wafanye kazi kwa kipindi kirefu zaidi na si kuogopa kwamba watatoroka jela.

Alimtaka mkuu mpya wa magereza ambaye alikuwa naye anaapishwa kama Kamishna Mkuu wa Magereza, Dk. Juma Ali Malewa, kuwapa mafunzo ya uhakika askari wake ili wawe na uwezo wa kuwalinda wafungwa vizuri.

Mabeyo amsifu Mwamunyange

Jenerali Mabeyo, Mkuu mpya wa majeshi, alisema ataendeleza kuimarisha taifa kiulinzi. Alisema JWTZ ina dhamana ya kulinda mipaka, wananchi na mali zao. Alisema ataanzia pale Jenerali Davis Mwamunyange alipoishia kwani alifanya kazi nzuri.

Aliahidi pia kuendelea kutatua migogoro iliyopo katika maeneo ya wananchi na jeshi.  Alisema wamekuwa wanafanya mazungumzo pale wanapoona kama wananchi waachiwe eneo na wanafanya hivyo.

 Jenerali Davis Mwamunyange aagwa rasmi

Baada ya kuapishwa Ikulu, Mkuu huyo wa Majeshi mpya aliwasili makao makuu ya Jeshi ambako alikagua gwaride na baadaye kufanyika tukio la kumuaga Mkuu wa Majeshi mstaafu, Mwamunyange, kwa gari lake kusukumwa mpaka nje ya geti na majenerali wa Jeshi hilo.

Jenerali Mabeyo alijiunga na Jeshi Januari 1, mwaka 1979 na kufanya mafunzo mbalimbali. Amewahi kuwa mwambata jeshi akiwakilisha JWTZ nchini Rwanda, msaidizi wa Mkuu wa Majeshi halafu kuwa Mkurugenzi Idara ya Usalama na Utambuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles