Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
HIVI karibuni katika mkutano wa pili wa biashara na ujasiriamali Afrika Mashariki uliofanyika Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wafanyabiashara wa Afrika Mashariki kutumia malighafi zinazopatikana miongoni mwa nchi wanachama kukuza uchumi wa viwanda.
Kwa mtazamo wake, anasema uagizaji wa malighafi za viwandani kutoka nje ya bara la Afrika unazorotesha ukuaji wa uchumi na kuwafanya wananchi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ambao wengi ni wakulima kuendelea kuishi maisha ya kimasikini.
“Tumekutana hapa leo kuangalia mambo ya kufanya kuelekea uchumi wa viwanda kwa kuangalia wapi tumefika, Serikali za Afrika Mashariki na sekta binafsi pia kuangalia imefika wapi katika utekelezaji wa azma hii muhimu katika maendeleo ya mataifa yetu.
“Ili tuendelee ni lazima viwanda vyetu vitegemee malighafi zinazozalishwa na wananchi katika jumuiya yetu, lakini pia tunaangalia suala la ajira kwa vijana wetu ambao kama tunavyofahamu ndilo kundi kubwa miongoni mwa watu wote katika jumuiya hii, ili viwanda hivi vinavyoanzishwa visaidie vijana hawa kupata ajira,” anasema Samia.
Anaamini kuwa ili wananchi wengi wafaidi keki ya Taifa, ni lazima kuunganishwa kwa nguvu ya pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi kwa kuanzisha viwanda vinavyotumia malighafi zinazotokana na mazao ya kilimo ambacho ni shughuli kuu ya kiuchumi kwa wananchi wengi hususan wanaoishi vijijini.
Anashauri kuanzisha viwanda vitakavyoongeza thamani kwenye kahawa, chai, pamba na mazao mengine, ili kupunguza kiasi kikubwa cha umasikini uliokithiri miongoni mwa wanajumuiya.
Anasema ikiwa Serikali za Afrika Mashariki zitashindwa kulipatia kipaumbele suala la ukosefu wa ajira na usawa wa kiuchumi, zitakuwa zinatengeneza bomu kubwa na hatari kwa jumuiya hiyo.
Anasisitiza kuwa kupitia shughuli za ujasiriamali, nchi wanachama wa jumuiya hiyo zinaweza kukuza uchumi wake, hivyo Serikali zinalo jukumu la kuingilia kati kuiunga mkono sekta binafsi kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia biashara ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu.
Kuhusu suala la uhakika anasema Serikali zote zina jukumu la kuangalia sheria zetu zinazosimamia mipaka na kuhakikisha uwepo wa amani ili kuwezesha biashara kufanyika katika mazingira salama, kuchochea kukua kwa uchumi unaohusisha watu wengi.
Vilevile Serikali zina jukumu la kuhakikisha zinawekeza katika mtaji wa watu kwa kuhakikisha zinatoa elimu itakayosaidia kupata wataalamu.
“Tuendelee kuboresha miundombinu na kuweka mazingira mazuri ya kufanyia biashara kwa kuhakikisha zinapatikana sheria zinazowalinda walaji na wazalishaji,” anasisitiza Samia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC), Lilian Awinja, anataja kugundulika kwa rasilimali kama vile mafuta na gesi kama moja ya sababu za kuvutia wawekezaji wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki sambamba na kuinua ukuaji wa sekta mbalimbali za kiuchumi.
Katika mkutano huo, wadau na wataalamu mbalimbali wa masuala ya viwanda na watunga sera walijumuishwa ili kuangalia changamoto zinazowakabili wajasiriamali na wafanyabiashara ndani ya jumuiya.
“Mkutano huu ni fursa nzuri ya kushawishi kupitiwa kwa sera, kuboreshwa kwa mazingira ya biashara na kuongeza kujiamini kibiashara na kuifanya Afrika Mashariki kuwa kitovu cha biashara duniani.
“Kuboreshwa kwa mazingira ya biashara kutaleta matokeo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupungua kwa gharama za kufanya biashara na kupanuka kwa soko la ushirikiano katika jumuiya,” anasema Lilian.
Mwenyekiti wa EABC, Jim Kabeho, anasisitiza kuongezwa nguvu katika kutangaza uwekezaji wa nje ya mikapa (CBI) na kuweka nguvu zaidi katika kushawishi wananchi wa Jumuia hiyo kutumia fursa zilizopo kukuza biashara zao.
Anasema kuwa ripoti ya biashara ya mwaka 2014, inaonesha kuwa Tanzania na Uganda ndizo zilizovutia uwekezaji mkubwa kutoka nje ya nchi, ambapo Tanzania ilivutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 104.1 (zaidi ya Sh bilioni 210), huku Uganda ikivutia dola milioni 75 (zaidi ya Sh bilioni 150).
Mwaka 2015 pekee Kenya ilivutia miradi 14 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola milioni 132.1 (zaidi ya Sh bilioni 296) kutoka katika nchi nyingine za jumuiya Afrika Mashariki, miradi mingi ikiwa ni kutoka nchini Rwanda.
Lakini taarifa nyingine inaonesha kuwa Kenya ilishuhudia kushuka kwa biashara miongoni mwa mataifa ya EAC kwa asilimia 10 kutoka Dola bilioni 5.6 mwaka 2014 hadi Dola bilioni 5.1 mwaka 2015.
Kushuka huko kunaweza kuwa kumesababishwa na sababu kadha wa kadha, ikiwamo kukosekana kwa utengamano wa kisiasa miangoni mwa nchi wanachama ambapo kwa vipindi tofauti baadhi ya nchi hizo zimekuwa katika migogoro baada ya uchaguzi kwa nchi kama Burundi, Rwanda na Uganda.
Vitisho ya ugaidi nchini Kenya kutoka kwa kundi la Al-Shabaab la nchini Somalia ambalo limekuwa likiishambulia nchi hiyo ya Mashariki mwa Afrika kama hatua ya kupinga majeshi ya Kenya kupelekwa nchini mwao.
Licha ya kuwa wajasiriamali wengi wa EAC ni wadogo na wa kati, wamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa jumuiya hiyo ambapo hutoa karibu asilimia 60 ya ajira rasmi na zisizo rasmi na wamekuwa uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi kwa tabaka la kati.
Sekta ya ujasiriamali huchangia asilimia 25 ya pato la ukanda huo, vilevile sekta hiyo huchukua asilimia 90 ya biashara zote zilizosajiliwa.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustino Mahiga, anasema ziko changamoto mbalimbali zinazotakiwa kutatuliwa ili kuwezesha biashara kufanyika kwa urahisi.
“Yako matatizo yasiyo ya kijumuiya, hayo tumekuwa tukiyazungumza kati ya nchi na nchi, kama sasa kuna hili suala la ng’ombe hilo si la Afrika Mashariki, kuna sheria na taratibu kwa sababu ng’ombe wanaongezeka kila siku hata sisi ndani tumeshuhudia migogoro ya wafugaji na wakulima, kwa hiyo tutakaa chini na kuliangalia,” anasema Balozi Mahiga.