Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), amesema ana kila sababu ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa sababu walimkopesha kura zao.
Alisema juhudi anazozifanya kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ilala na vikao mbalimbali vya Bunge ni kutafuta ufumbuzi wa kero mbalimbali za wananchi waliompigia kura kwa ahadi ya kuwaletea maendeleo.
Alikuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara Mtaa wa Kiombo Kata ya Kitunda jimboni humo.
Alisema atahakikisha kila fedha inayopatikana inapelekwa kwenye miradi ya wananchi kadri iwezakanvyo kupunguza kero sugu zinazowakabili wapiga kura wake.
“Leo ilikuwa siku maalum ya kuzindua mradi wa zahanati kwa ajili ya wagonjwa wa Kifua Kikuu (TB), maabara mbili Shule ya Sekondari Kitunda na daraja la Kiombo… hizi ni ahadi nilizozitoa wakati naomba ubunge.
“Miradi niliyoizindua leo ni sehemu ya deni walilonikopesha wananchi, tutaendelea kupunguza kero hizi kwa kutumia kila aina ya senti inayopatikana kuzipunguza,” alisema Waitara.
Mbunge huyo aliwaonya watendaji wa Halmashauri ya Ilala watakaochelewesha miradi ya wananchi kwamba wataondolewa na hata wakandarasi watanyang’anywa miradi hiyo.
Hata hivyo alionyesha wasiwasi wa kushuka mapato ya halmashauri hiyo baada ya Serikali kuhamishia ukusanyaji kodi ya majengo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Utaratibu wa Serikali kuhamishia fedha za majengo kwa TRA kutazifanya halmashauri kuwa hohehahe na kushindwa kukopesheka kwa sababu mapato yake yameporomoka kwa kiasi kikubwa,”alisema.
Katika mkutano huo wa hadhara baadhi ya wananchi walieleza kero zao zikiwamo ukosefu wa soko, usafiri wa Kitunda hadi Kariakoo, Muhimbili na Posta kurahisisha shughuli zao.