31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wahariri wauchana muswada wa habari

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Theophil Makunga, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari. Katikati ni Katibu wa Jukwaa hilo, Neville Meena na Mjumbe wa Jukwaa, Bakari Machumu (kulia).
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Theophil Makunga, akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari. Katikati ni Katibu wa Jukwaa hilo, Neville
Meena na Mjumbe wa Jukwaa, Bakari Machumu (kulia).

Na Patricia Kimelemeta, DAR E SALAAM

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limeuchambua kwa kina Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 na kusema kuwa una mapungufu mengi ambayo yanahitaji maoni ya kina ya wadau.

Vilevile wameliomba Bunge kutouharakisha kuuwasilisha sasa na badala yake uwasilishwe katika Bunge la Februari mwakani baada ya kufanyika kwa marekebisho hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema wamepeleka ombi la kusogezwa mbele kuwasilishwa muswada huo kwa Bunge, lakini bado upande wa mmoja wa Serikali umekuwa ukipambana kuhakikisha unawasilishwa huku maoni ya wadau yakikosekana.

Makunga alisema muswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza Septemba mwaka huu lakini bado kuna kasoro kadhaa katika baadhi ya vifungu kuanzia cha 12 hadi 55.

Alisema vifungu hivyo   vinaonekana kuwakandamiza wanahabari katika kutekeleza majukumu yao hali ambayo inaweza kuhatarisha na kuua taaluma ya habari nchini.

“Hatuwezi kuizuia Serikali kuwasilisha muswada bungeni katika kikao kinachoanza kesho kwa sababu wao ndiyo wenye uamuzi.

“Lakini pia bado tuna nafasi ya kuwaomba wasogeze hadi Februari mwakani  wadau waweze kuupitia na kutoa maoni yao.  Tunaamini kwa kufanya hivyo tunaweza kupata sheria bora ambayo itabeba masilahi ya wanahabari nchini,” alisema Makunga.

Mwenyekiti huyo wa TEF alisema   kinachofanywa na serikali ni kutekeleza wajibu wao wa katiba na sheria na TEF haina dhamira ya kukwaza utunzi wa sheria na wala kupinga kutungwa   sheria hiyo.

Alisema licha ya hali hiyo, bado kuna nafasi ya kuujadili muswada huo kwa kina ili kupata mawazo mbalimbali ambayo yatabeba dhima ya Sheria ya Habari nchini.

“Ikiwa Serikali itashindwa kukubali ombi letu na kuamua kuupitisha muswada huo ambao kama wanahabari tunaona unakandamiza tasnia katika baadhi ya vipengele, tutashirikiana na wanasheria kuangalia vipengele vyenye matatizo na kwenda mahakamani kuvipinga,” alisema.

Akianisha vipengele  vinavyoonekana kandamizi kwenye muswada huo, Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema ni pamoja na kifungu cha 12 ambacho kimeipa mamlaka bodi kufanya ithibati na kutoa Press Card, wakati kazi hiyo inaweza kutolewa na Baraza Huru la Habari.

“Kifungu cha 13(a) kinasema   mwandishi akishaondolewa katika orodha ya wanahabari haruhusiwi kufanya kazi kwenye chombo chochote cha habari au taaluma inayohusiana na mambo hayo, jambo linaloonyesha wazi kuwa uamuzi huo ni wa kummaliza mwanahabari hata kama alifanya kosa kwa bahati mbaya,” alisema Balile.

Kingie ni   kifungu cha 47 ambacho kinasema mwanahabari atakayekutwa na kosa anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano hadi 20 au kifungo cha miaka mitatu jela au kisichopungua miaka mitano.

“Na kifungu cha 50 kinasema mtu yeyote yule hata kama siyo mwanahabari atakayekutwa na chapisho la uasi anatakiwa kulipa faini ya Sh  milioni mbili au isiyozidi Sh milioni tano na ikiwa amerudia kosa hilo atafungwa miaka mitatu jela.

“Mbali hilo na pia kifungu cha 55 katika muswada huo kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana kufuta chombo chochote cha habari huku Kifungu cha 60 (a) Waziri anatakiwa kutunga kanuni ya utoaji wa taarifa ya vyanzo vya mapato kwa vyombo vya habari wakati vyombo hivyo baadhi yao vinamilikiwa na watu binafsi,”alisema Balile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles