Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekumbwa na kashfa kubwa baada ya watu wawili wanaodaiwa kuwa wahalifu sugu kutoroka katika Kituo cha Polisi Kurasini usiku wa kuamkia juzi.
Watuhumiwa hao, wanadaiwa kushiriki matukio makubwa ya uhalifu ambayo yametikisa nchi katika siku za hivi karibuni.
Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata jana kutoka kwenye vyanzo vyake ndani ya jeshi hilo, zinasema watuhumiwa hao walikuwa watatu, lakini waliofanikiwa kutoroka ni wawili.
Chanzo chetu kilisema kuwa mtuhumiwa mmoja alikamatwa wakati akiwa kwenye harakati za kukimbia.
“Kuna wahalifu wawili wametoroka usiku wa kumkia jana (juzi), wanadaiwa kuhusika katika matukio mbalimbali ya kiuhalifu.
“Hatujui wamekimbilia wapi, nakuhakikishia polisi watawatia mbaroni tu.
“Sina uhakika, lakini ninavyojua polisi watakuwa wameanza msako mkali,” kilisema chanzo chetu.
Alipotafutwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu ili kutoa ufafanuzi wa tukio hilo, alimtaka mwandishi wetu kuwasiliana na kamanda wa mkoa husika au Kamishina wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
“Sina taarifa ya kuwapo tukio hili, nakuomba uwasiliane na makamanda wahusika au Kamanda Kova watakusaidia,” alisema IGP Mangu.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkodya ili kutoa ufafanuzi wa tukio hilo, alisema hadi jana jioni hakuwa na taarifa hizo, lakini alimtaka mwandishi wa gazeti amtafute Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke kwa ufafanuzi zaidi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alipoulizwa kuhusu kutoroka kwa watu hao, alisema hakuna tukio kama hilo.
Alisema huo ni uvumi tu wa watu, pia hakuna operesheni iliyofanyika hivi karibuni ya kuwakusanya watu zaidi ya 30 na kama ni wahalifu sugu wanakaa gerezani na si kituoni.
“Ndugu mwandishi, kwanza unaposema kuwa wahalifu hao walitoroka katika Kituo cha Polisi Kurasini ambacho ni maalumu kwa wahalifu sugu, kwa kweli hatuna kituo kama hicho.
“Hata kama tumefanya operesheni maalumu ya kuwakamata wahalifu katika mikoa yote, hatuwezi kuwaweka idadi kubwa ya wahalifu eneo moja.
Naye Naibu Kamishina wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tukio hilo, alisema yeye hana mamlaka ya kuzungumza kwa sababu mzungumzaji yupo.
Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamisha Suleimani Kova, alisema taarifa hizo