Na WANDISHI WETU
WAGOMBEA udiwani 45 kutoka vyama vitatu vya upinzani wameenguliwa kutokana na sababu mbalimbali, hali inayofanya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa kwenye nafasi ya kushinda viti vingi kati ya 77 vinavyogombewa kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Agosti 12.
Wagombea hao 16 wanatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), 9 wanatoka Chama cha Wananchi (CUF) na 20 Chama cha ACT – Wazalendo.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, Mkurugenzi wa Itikadi na Uenezi wa Chadema, John Mrema, alisema hadi kufika jana, wagombea udiwani 16 wa chama hicho wameenguliwa kwenye uchaguzi huo.
Kwa upande wa CUF, inayomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma, Abdul Kambaya, alisema wagombea 9 wa chama hicho wameenguliwa, huku kwa upande wa Chama cha ACT- Wazalendo, Ofisa Habari wake, Abdallah Khamis, akisema wagombea 20 wameenguliwa.
Miongoni mwa sababu ambazo zilitajwa kusababisha wagombea hao kuenguliwa kwenye mchakato huo, ni kutojua kusoma, kukosea kujaza fomu, mihuri kugongwa juu ya picha na wengine kujitoa wenyewe.
Hali hiyo, imefanya Chadema kuomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutaka uchaguzi usogezwe mbele, ili malalamiko yao yashughulikiwe.
Wakati tume ikiwa haijatoa majibu ya suala hilo, jana Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Longido, Juma Mhina, alimwengua Mgombea wa Chadema wa Kata ya Kamwanga, Sakimba Nakutamb, baada ya pingamizi alilowekewa na mgombea wa CCM.
Akizungumzia kuhusu pingamizi hilo, Mhina alisema: “Mgombea alishindwa kujaza fomu namba10, hata alipopelekewa barua ya pingamizi hakuweza kuijibu hadi muda aliotakiwa kuresha majibu ofisini ulipomalizika. Kutokana na pingamizi hilo, mgombea wa CCM kwenye Kata hiyo, Elias Laizer, amepita bila kupingwa.”
Alisema katika uchaguzi huo, kata itakayofanya uchaguzi ni Olmolog pekee, ambayo Lomayani Laizer anagombea kwa tiketi ya CCM na Philipo Leng’ochai kwa tiketi ya Chadema.
Alisema katika kata za Langatadapash na Kamwanga, wagombea wa CCM wamepita bila kupingwa, baada ya wagombea wa upinzani kushindwa kukidhi vigezo na kuwekewa pingamizi.
Hali hiyo ni mwendelezo wa wagombea wa upinzani kung’olewa. Alhamisi wiki hii mgombea udiwani wa Kata ya Mpona (Chadema), Iskaka Mlonge, alienguliwa baada ya msimamizi wa uchaguzi kujiridhisha na mapingamizi yaliyotolewa na mgombea wa CCM, Michael Siwingwa, aliyedai kuwa Mlonge si raia.
Kutokana na wagombea wengi wa Chadema kuenguliwa, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa chama hicho, Reginald Munisi, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kusitisha uchaguzi kwenye baadhi ya maeneo na kuanza upya mchakato wa kupata wagombea, ili kila mtu mwenye haki apate nafasi hiyo.
Alibainisha maeneo ambayo chama hicho kinaona kimeonewa ni Tunduka, kwenye kata tano, ambako wagombea walinyimwa fomu.
Alisema kwa Mkoa wa Arusha, mgombea kwenye Kata ya Teratu alinyang’anywa fomu mbele ya msimamizi wa uchaguzi.
Na kwa Mkoa wa Iringa alidai wasimamizi katika kata mbili za Gangilonga na Kilosa walikataa kupokea fomu za wagombea wa Chadema, mazingira ambayo aliyaeleza kuwa yanawatengenezea ushindi wagombe wa CCM.